1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pence akutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya na NATO

Josephat Charo20 Februari 2017

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence anakutana (20.02.2017) na viongozi wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya NATO Brussels katika awamu ya mwisho ya ziara yake Ulaya kuwahakikishia ushirikiano washirika.

https://p.dw.com/p/2XtY6
Belgien USA Charles Michel & Mike Pence in Brüssel
Makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence (kushoto) alipokutana na waziri mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel (19.02.2017)Picha: Getty Images/AFP/N. Maeterlinck

Pence alisema Umoja wa Ulaya na Marekani zina maadili yanayofanana na Marekani itaendelea kujitolea kwa dhati kutimiza malengo yaliyowekwa na pande hizo mbili. "Lazima tuwe imara na tuungane katika kuvikabili vitisho dhidi ya usalama na uthabiti barani Ulaya," aliongeza kusema.

Kiongozi huyo aliutaka Umoja wa Ulaya kujiunga na Marekani katika kuongeza juhudi za kupambana na wanamgambo wa kiislamu barani Ulaya na Marekani itaendelea kubakia mshirika kamili wa Umoja wa Ulaya na nchiw ashirika barani humo katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Baada ya kuwasili mjini Brussels hapo jana Pence alisema anasubiri kwa hamu kubwa mikutano yake na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, rais wa baraza la Ulaya, Donald Tusk, rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jean Claude Juncker, na katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jens Stoltenberg.

NATO-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATOPicha: Reuters/F. Lenoir

"Ni heshima kubwa kuwa nanyi hapa Brussels. Nina matarajio makubwa katika mikutano yangu na viongozi wa Umoja wa Ulaya pamoja na viongozi wa jumuiya ya kujihami ya NATO," alisema Pence.

Pence aliwasili Brussels akitokea mjini Munich Ujerumani ambako alihudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu usalama. Katika mkutano huo Pence aliwaambia viongozi wa Ulaya na wataalamu wa masuala ya ulinzi kwamba Marekani daima itakuwa mshirika wao mkubwa. Pence aidha alisema rais Trump na Wamarekani wote wamejitolea kwa dhati kwa uhusiano baina ya Marekani na Ulaya.

Hatua ya rais Trump kuikosoa jumuiya ya NATO akisema imepitwa na wakati, kuupongeza uamuzi wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya na msimamo wake unaoonekana kuegemea upande wa rais wa Urusi, Vladimir Putin, imewatia tumbo joto washirika wa Marekani barani Ulaya. Na nchi washirika zinaendelea kutafuta hakikisho licha ya kwamba Pence, waziri wa ulinzi wa Marekani, James Mattis na waziri wa mambo ya nchi za nje, Rex Tillerson, wana uzoefu wa miaka mingi na sera kuhusu ushirikiano kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya wakati walipokuwa wakihudumu barani Ulaya.

Deutschland Münchner Sicherheitskonferenz 2017 Federica Mogherini
Federica Mogherini, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa UlayaPicha: Reuters/M. Rehle

Pence alisema Marekani itaishinikiza Urusi iuheshimu mkataba wa Minsk kuhusu mzozo nchini Ukraine na Tillerson kwa upande wake alisema Marekani itashirikiana na Urusi iwapo tu ushirikiano huo utawanufaisha Wamarekani.

Mahusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani kukwama

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, alisema ameshangazwa kwamba Pence hakuutaja Umoja wa Ulaya katika hotuba yake, na hivyo kuibua wasiwasi baada ya rais Trump kuyakaribisha matokeo ya kura ya maoni iliyoiondoa Uingereza kutoka kwa Umoja wa Ulaya, Brexit, na kuonekana akiwa na matumaini kwamba nchi nyingine zitafuata mkondo huo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, amesema ziara ya Mike Pence mjini Brussels ni ishara muhimu sana kisiasa ingawa amependekeza mahusiano baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani yanaweza kuvurugika kidogo na kukwama kiasi fulani ikilinganishwa na ilivyokuwa kabla Trump kuingia madarakani.

Tusk na Juncker, ambao watakutana na Pence kwa mara ya kwanza, pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu rais Trump. Juncker alisema baada ya Trump kushinda uchaguzi kwamba ana hofu huenda akatekeleza yote aliyoyasema wakati wa kampeni.

Huku mkutano kati ya Pence na viongozi wa Umoja wa Ulaya na NATO ukitarajiwa kuwa wa kidiplomasia, makundi kadhaa yanapanga kufanya maandamano dhidi ya sera za rais wa Marekani, Donald Trump.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/reuters/ape

hariri: Mohammed Abdul-Rahman