1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pence aionya Korea kaskazini

Sekione Kitojo
18 Aprili 2017

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence ameihakikishia Japan kuwa Marekani inasimama kwa asilimia 100 nyuma yake mshirika mkuu katika eneo la Asia katika juhudi za kuzuwia kitisho kutoka Korea kaskazini.

https://p.dw.com/p/2bNke
Südkorea Besuch US Vizepräsident Mike Pence PK mit Hwang Kyo Ahn
Makamu wa rais Mike Pence (kushoto) pamoja na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe (kulia)Picha: Getty Images

Pence  alizungumza  kwa  maneno  makali  wakati  akianza mazungumzo  na  waziri  mkuu  wa  Japan Shinzo  Abe pamoja  na  viongozi  wengine  wa  Japan  baada  ya kuwasili  katika  kituo  cha  jeshi  la  Marekani  akitokea Korea  kusini.

"Tunatambua hali  ngumu  ambayo  watu  wa  Japan wanapitia  kutokana  na  uchokozi  unaofanywa  kutoka upande  wa  pili  wa  bahari  ya  Japan," Pence  amesema , na  kuongeza  "tuko  nanyi  kwa  asilimia  100."

Japan Besuch Mike Pence Handschlag mit Abe
Makamu wa rais Pence(kushoto) akiwa na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe(kulia) katika mazungumzo Picha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Utawala  wa  rais  Donald Trump umeashiria  kuchukua mtazamo wa  nguvu  zaidi  kutokana  na  majaribio  ya  hivi karibuni  ya  makombora  ya  Korea  kaskazini  na  vitisho, ikiwa  ni  pamoja  na  onyo  kutoka  kwa  Trump  kwamba kiongozi  wa  Korea  kaskazini Kim Jong Un, anapaswa , "awe na  adabu."

Jana  Jumatatu , Pence  alisafiri  kwenda  katika  eneo ambalo  limetengwa  bila  kuwa  na  shughuli  za  kijeshi , linalotenganisha  Korea  kaskazini  na  kusini , ambako alimuonya  kiongozi  wa  Korea  kaskazini  kwamba  baada ya   nchi  hiyo  kuijaribu  Marekani  na  Korea  kusini  kwa dhamira  yake  ya   kujipatia  silaha  za  kinyuklia, "enzi za mkakati  wa  uvumilivu zimekwisha."

Südkorea Besuch US Vizepräsident Mike Pence
Makamu wa rais wa Marekani akiwa katika eneo lililotengwa lisilikuwa na shughuli za kijeshi kati ya Korea kaskazini na kusini.Picha: Reuters/K. Hong-Ji

Marekani yaitaka China kutumia  ushawishi wake

Pence  akiwa  katika  ziara  ya  siku  10  ya  mataifa  ya Asia  ambayo  pia  itamfikisha  nchini  Indonesia  na Australia , amesema  Trump  ana  matumaini  China itatumia  ushawishi  wake  kuwezesha  mshirika  wake huyo  wa  karibu  kuachana  na  dhamira  yake  ya mpango  wa  kinyuklia. Abe kwa  upande  wake  amesema anamatumaini  ya mazungumzo  ya  amani  na Pyongyang, lakini  wakati  huo  huo  akaongeza , mazungumzo  kwa  nia  ya  mazungumzo  tu  hayana maana.

Nordkorea Machthaber Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong UnPicha: picture-alliance/AP Images/W. Maye-E

"Ni  dhahiri  kwamba, hili  ni  suala  la  umuhimu  wa  juu kabisa  kwetu kutafuta juhudi za  kidiplomasia pamoja  na suluhisho la  amani  la  suala  la  Korea kaskazini. Lakini wakati  huo  huo , mazungumzo kwa  ajili  tu  ya mazungumzo  hayana  maana  na  ni  muhimu  kwetu kuweka  mbinyo dhidi  ya  Korea  kaskazini ili iweze kujitokeza  na  kufanya  mazungumzo yenye  maana."

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  China Wang Yi  ametoa wito  mpya  leo  wa  utulivu katika  rasi  ya  Korea. Wang amewaambia  waandishi  habari  kwamba  licha  ya  kuwa maafisa  wa  Marekani  wameweka  wazi  kwamba shambulio  la  kijeshi  linawezekana, anamini  kwamba marekani  bado  itapendelea  kupunguza wasi wasi  kupitia mazungumzo  yatakayohusisha  pande  zote.

China PK französischer Außenminister Jean-Marc Ayrault und Wang Yi in Beijing
Waziri wa mambo ya kigeni wa China Wang YiPicha: Reuters/J. Lee

Wakati huo  huo  Korea kaskazini imesema  itaendelea kufanya  majaribio  ya  silaha  zake  kila  wakati  na  hatua yoyote  ya  kijeshi  dhidi  yake  itazusha  vita  kamili , amesema  afisa mwandamizi  wa  Korea  kaskazini alipozungumza  na  BBC.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo