1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pembe ya Afrika yasifiwa kwa maendeleo kisiasa na kiuchumi

Lubega Emmanuel/DW Kampala29 Novemba 2018

Wajumbe wa ngazi za juu kutoka Umoja Mataifa pamoja na shirikisho la maendeleo la pembe ya Afrika IGAD wamesifu mabadiliko katika kanda hiyo kuhusiana na masuala ya siasa, usalama na uchumi hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/398zs
Äthiopien Friedensverhandlungen über Südsudan in Addis Ababa
Picha: ZACHARIAS ABUBEKER/AFP/Getty Images

Wajumbe wa ngazi za juu kutoka Umoja Mataifa pamoja na mamlaka ya shirikisho la maendeleo la pembe ya Afrika IGAD wamesifu mabadiliko yanayoshuhudiwa katika kanda hiyo kuhusiana na masuala ya siasa, usalama na uchumi hivi karibuni. Kwenye mkutano wao wa kutathimini utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili uliosainiwa mwaka 2015 nchini Djibouti, wawakilishi wa nchi za eneo hilo pamoja na maafisa wa Umoja Mataifa wamewapongeza viongozi wa kisiasa hususan waziri mkuu wa Ethiopia kwa kuchapua utekelezaji wa mkataba huo.

Hadi mwaka 2015, kanda ya pembe ya Afrika hasa nchi zinazopakana na Ghuba ya Arabuni zimekumbwa na hali mbaya ya usalama na hivyo kutumiwa na makundi ya magaidi kuendesha harakati zao. Uchumi wa nchi hizo ulikuwa umezorota kabisa kutokana pia na uhasama wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa nchi za Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini na Somalia.

Lakini wimbi jipya la mabadiliko limeshuhudiwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu tangu kusainiwa kwa mkataba kati ya Umoja Mataifa na Mamlaka ya Shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika, IGAD. Chini ya mkataba huo, viongozi na wanasiasa wa nchi hizo waliahidi kutumia njia za mazungumzo na upatanisho ili kutatua mizozo wakifahamu kuwa kuzorota kwa amani kunaathiri maendeleo ya kanda hiyo. Wajumbe wa ngazi za juu wa pande zote mbili wamekutana kutathimini mafanikio na changamoto katika kutekeleza mkataba huo. Balozi Maboub Maalim ni katibu mtendaji wa IGAD.

Wimbi jipya la mabadiliko limeshuhudiwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu tangu kusainiwa kwa mkataba kati ya Umoja Mataifa na Mamlaka ya Shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika, IGAD
Wimbi jipya la mabadiliko limeshuhudiwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu tangu kusainiwa kwa mkataba kati ya Umoja Mataifa na Mamlaka ya Shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika, IGAD

Wajumbe wamemtaja waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuwa nguzo muhimu katika kuondosha uhasama wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu miongoni mwa nchi za pembe ya Afrika na badala yake kuzindua mikakati ya kujenga mahusiano mema na yenye tija kwa raia wa kanda hiyo. 
 

Pembe ya Afrika inapakana na ghuba ya Arabuni ambako harakati za kigaidi na zinazidi kutatiza amani na usalama. Hivyo kuna wasiwasi kuwa hali hii itaathiri juhudi za kuleta amani ya kudumu katika mataifa ya Somalia,Eritrea na Djibouti ambayo pwani zake zingekuwa kichocheo muhimu cha kuvutia uwekezaji. Changamoto hiyo pamoja na zingine ndizo Mratibu wa Umoja mataifa wa mkataba huo Rosa Malango anataka zizingatiwe na wajumbe katika mkutano wao utakaokamilika kesho Ijumaa.
 

Wajumbe wamewataka viongozi wa Sudan Kusini kuheshimu mkataba waliosaini mwezi Septemba mwaka huu kuwezesha raia wao kurejelea maisha ya kawaida. Mchakato wa mazungomzo uliofanikisha mkataba huo ulisimamiwa ba viongozi wa nchi za IGAD.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Mohammed Khelef