Pelosi kutuma ibara za mashtaka kwa Seneti
10 Januari 2020Uamuzi huo unaweza kupunguza mvutano na maseneta wa chama cha Republican waliochukizwa na hatua ya kuchelewa kwa shauri hilo.
Spika Pelosi anakabiliwa na shinikizo kutoka Warepublican na baadhi ya wanachama wa Democrat la kumtaka asitishe mpango wake wa kuchelewesha shauri dhidi ya Trump mbele ya baraza la Seneti wiki tatu tangu Baraza la Wawakilishi lilipopitisha uamuzi wa kumshtaki rais kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka na kuzuia upatikanaji haki.
Pelosi alichukua uamuzi huo kutokana na wasiwasi kuwa Baraza la Seneti linalodhibitiwa na chama cha rais Trump cha Republican litafikia hitimisho la kumuondolea mashtaka kiongozi huyo hata kabla ya shauri dhidi yake kusikilizwa.
Pelosi: Tuko tayari kupeleka ibara hizo
Akizungumza na waandishi habari mjini Washington jana, Pelosi amesema hana mipango ya kuzuia ibara za mashtaka bila kikomo lakini alihitaji taratibu za uendeshaji shauri hilo mbele ya Seneti ziwekwe wazi kwa umma
"Tuko tayari. Tunajisifu kwa kuilinda kwetu katiba ya Marekani. Tuna wasiwasi kwamba maseneta hawatoweza kutimiza kiapo chao kwa kuendesha shauri chini ya misingi ya kutoegemea upande wowote. ni ngumu kwao" amesema Pelosi
Wengi katika bunge la Marekani wanataraji shauri la mashtaka dhidi ya rais litaanza mapema wiki inayokuja.
Mvutano kati ya Spika Pelsosi na kiongozi wa walio wengi kwenye Baraza la Seneti Mitch McConnell unaonekana kuwa jaribio la kupimana ubavu kati ya pande mbili za bunge la Marekani kuelekea kisa cha tatu cha kumfungulia mashatka rais wa taifa hilo kaitka historia.
Baraza la Wawakilishi wamfunga mikono Trump
Katika hatua nyingine Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani limepitisha azimio la kuzuia uwezo wa Rais Donald Trump wa kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran bila ridhaa ya baraza la Congress.
Azimio hilo lisilo na nguvu kisheria linamtaka Rais Trump kusitisha mipango yote ya kijeshi dhidi ya Iran hadi pale bunge litakapoidhinisha kuingia vitani na nchi hiyo au kuruhusu kutumika nguvu kudhibiti shambulzii dhidi ya Marekani.
Wiki iliyopita, Trump alitoa idhini ya kuuliwa kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran, Qassem Soleimani, kisa kilichozusha hasira kutoka kwa wajumbe wa Democrat na baadhi ya wale wa Republican waliohoji sababu na uzito wa kufikia uamuzi huo.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema licha ya kwamba azimio hilo halina nguvu kisheria, lakini ni ujumbe wa wazi kwa Rais Trump kwa sababu linaakisi msimamo wa wabunge.