1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pele aendelea kupata nafuu hospitalini

28 Novemba 2014

Mchezaji wa kandanda nguli wa Brazil Pele, ambaye amekuwa hospitalini kwa siku nne kutokana na maambukizi ya njia ya mkojo, amesema kuwa anaendelea kupata nafuu.

https://p.dw.com/p/1Dwee
Brasilien Fußball Pele
Picha: picture-alliance/dpa/B. Zborowski

Awali hospitali alikolazwa ya Albert Einstein mjini Sao Paolo ilisema kuwa hali yake “imeimarika” na kuwa gwiji huyo mwenye umri wa miaka 74 – anayetambulika kama mchezaji bora zaidi katika historia – anapata matibabu kuhusiana na matatizo ya figo.

Pele amesema kwenye ukurasa wake wa Facebook na Twitter kuwa anaendelea vyema na anajihisi vyema kutokana na mapenzi ya mashabiki wake. Alisema alihamishiwa chumba maalum kwa sababu alihitaji kuwa katika mazingira ya faragha, ili aweze kuendelea kupata nafuu kwa amani.

Pele alifanyiwa upasuaji wa kuisafisha figo mnamo Novemba 13. Miaka miwili iliyopita, Novemba 15, 2012, Pele alifanyiwa upasuaji wa nyonga katika hospitali hiyo.

Katika taaluma yake ya kandanda alifunga magoli 1,281 katika mechi 1,363. Alifunga mabao 77 katika mechi 91 za timu ya taifa na akashinda Kombe lake la kwanza la Dunia akiwa na umri wa miaka 17, alipofunga mabao mawili katika fainali ya mwaka wa 1958 dhidi ya wenyeji Sweden. Katika mwaka wa 1977, aliisaidia klabu ya New York Cosmos kushinda ubingwa wa ligi ya Marekani katika msimu wake wa mwisho na klabu hiyo iliyokuwa pia na wachezaji wengine maahiri Franz Beckenbauer, mshambuliaji wa Italia Giorgio Chinaglia na nahodha wa zamani wa Brazil Carlos Alberto.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo