Paris.UNIFIL kuenda Lebanon baada ya siku kumi.
31 Agosti 2006Vikosi vya kijeshi vya Israel vitaanza kuondoka kusini mwa Lebanon mara tu wanajeshi elfu tano wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi kumi na sita elfu wa Lebanon watakapochukua nafasi zao nchini humo.
Akizungumza na kituo cha radio cha Ufaransa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amenukuliwa akisema kuwa kuwa, hilo ndilo suala alilolizungumza na serikali ya Israel.
Aidha Annan amesema, katika mazungumzo hayo wamekubaliana kupelekwa kwa kiasi hicho cha wanajeshi huko kusini mwa Lebanon na ndipo Israel itaondosha vikosi vyake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, anamatumaini ndani ya wiki moja ama siku kumi, Umoja huo utatuma vikosi hivyo na kuilazimisha Israel kuondosha majeshi yake nchini humo.
Hata hivyo hapo jana mkuu wa tume ya kusimamia amani wa umoja wa mataifa Jean-Marie Guehenno alisema kuwa jeshi la kulinda amani litakalokwenda nchini Lebanon UNIFIL litakuwa na wanajeshi kati ya elfu nne na elfu tano na litakuwa tayari limeshawekwa hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi September.