1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

Paris yanga'a wakati wa ufunguzi wa michezo ya Olimpiki

27 Julai 2024

Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2024 imefunguliwa mjini Paris kwa mbwembwe na mtindo wa kipekee huku mamia ya wanariadha washiriki wakiabiri maboti katika mto Seine katikati ya burudani la kukata na shoka la muziki.

https://p.dw.com/p/4ioSu
Ufaransa | Paris 2024 | Zinedine Zidane
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa Zinedine Zidane akishika mwenge wakati wa sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.Picha: LOIC VENANCE/Pool via REUTERS

Hafla hiyo ya ufunguzi imetoa fursa adimu ya kuuonyesha utamaduni wa Ufaransa, fasheni na muziki japo ilikumbwa na kiwingu cha mvua. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, hafla ya ufunguzi haikufanyika ndani ya uwanja kama ilivyozoelekea bali kwenye Mto Seine katikati ya mji mkuu Paris.

Wanamuziki tajika duniani Celine Dion, Lady Gaga, nyota wa muziki wa RnB Aya Nakamura miongoni mwa wengine walitumbuiza maelfu ya mashabiki waliostahamili kishindo cha mvua ili kushuhudia moja kati ya ufunguzi wa hafla kubwa za michezo duniani.

Soma pia:  Polisi ya Ufaransa imeihakikishia Israel usalama wakati wote wa Olimpiki

Zaidi ya wakuu 100 wa nchi walihudhuria hafla hiyo ya ufunguzi akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mke wa Rais wa Marekani Jill Biden miongoni mwa viongozi wengine.

Usalama waimarishwa kila kona ya Paris

Hii ni mara ya kwanza katika muda wa miaka 100 kwa Paris kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki ya majira ya joto huku michezo hiyo ikiandaliwa ndani au karibu na maeneo mashuhuri na yaliobeba historia pana ya mji mkuu huo wa Ufaransa.

Michezo hiyo ya Paris ni ya kwanza kuwiana na mageuzi ya kamati ya Olimpiki IOC kwa kupata usawa wa kijinsia miongoni mwa wanamichezo washiriki: wanariadha wa kiume 5,250 na idadi sawa na hiyo ya wanawake watamwaga kijasho kupigania dhahabu, fedha na shaba kwa heshima ya timu zao za taifa.

Paris2024 Olympische Spiele
Maafisa wa usalama wakifanya ukaguzi kabla ya sherehe za ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya majira ya joto 2024.Picha: Andy Wong/AP/picture alliance

Takriban maafisa wa polisi 45,000 na maelfu ya wanajeshi wameshika doria wakati wa hafla hiyo ya ufunguzi.

Polisi wengine nao walishika doria kandokando mwa mto Seine, yote hayo kwa ajili ya kumpa shabiki utulivu wa nafsi.

Maafisa wamewaondolea hofu mashabiki huku wakisema hali ya usalama imeimarishwa kwa kiwango cha juu na kwamba hakuna kitisho chochote aidha katika hafla ya ufunguzi au wakati michezo hiyo itakapokuwa inaendelea.

Kiwingu cha mizozo ya Ukraine na Gaza

Hata hivyo, tangu makala ya 32 ya Olimpiki majira ya baridi yalioandaliwa mjini Beijing China, kumeibuka mizozo nchini Ukraine na katika ukanda wa Gaza na hivyo kuzua wasiwasi wa kimataifa.

Wanamichezo kutoka Israel wanalazimika kupewa ulinzi mkali kwa saa 24.

Wanariadha wa Urusi na Belarus wamepigwa marufuku kushiriki michezo hiyo ya Olimpiki ingawa 15 kutoka Urusi na wengine 17 wa Belarus wamejumuishwa kushiriki lakini kama wanariadha huru na wasiogemea taifa lolote.

Ufaransa | Paris 2024 | Olimpiki Paris
Bendera za nchi zitakazoshiriki ya Olimpiki zikiwasili katika ukumbi wa Place du Trocadero.Picha: Edgar Su/REUTERS

Makala hiyo ya 33 ya michezo ya Olimpiki inafanyika chini ya kiwingu cha hali mbali ya kisiasa nchini Ufaransa japo kuwaondolea hofu wanamichezo washiriki, Rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach amewaeleza wanamichezo hao kuwa, wao ni sehemu ya hafla muhimu inayounganisha ulimwengu kwa amani.

Soma pia: Olimpiki: Kenya yaandamwa na kivuli cha kututumua misuli

Michezo hiyo itakayoshirikisha fani 32 na zaidi ya mataifa 200, itadumu kwa muda wa siku 19, na itafunga pazia lake mnamo Agosti 11.

Wanamichezo washiriki kutoka barani Afrika wanataraji kuvuna ushindi na kuliletea sifa bara hilo. Katika michuano ya soka, Misri, Guinea, Mali na Morocco zimebeba matumaini ya Afrika katika michezo hiyo ya Olimpiki.