PARIS: Umoja wa Ulaya wataka mkataba mpya wa hali ya hewa ushughulikiwe.
3 Februari 2007Umoja wa Ulaya umetoa wito mashauriano ya kimataifa yaanzishwe kuhusu mkataba mpya wa kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Mazingira, Stavros Dimas, alitoa wito huo jana mjini Paris, baada ya jopo la Umoja wa Mataifa kutoa taarifa ya tathmini yake ya ongezeko la hali ya joto duniani.
Taarifa hiyo inaarifu asilimia tisini ya mambo yanayosababisha hali ya joto kuongezeka duniani yametokana na shughuli za binadamu, na athari zake zitakuweko kwa karne nyingi zijazo.
Jopo hilo linalojumuisha wataalamu elfu mbili na mia tano kutoka mataifa zaidi ya mia moja na thelathini limetabiri kwamba ukame utaongezeka, kutakuwa na vipindi virefu vya joto na pia kuinuka usawa wa maji ya bahari .
Jopo hilo linasema athari za mabadiliko ya hali ya hewa huenda zitadumu kwa miaka zaidi ya elfu moja hata kama gesi zinazotoka viwandani zitapunguzwa.