1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Kikao cha ufadhili wa Lebanon chaanza nchini Ufaransa.

25 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCY4

Kikao cha wafadhili kimeanza Paris nchini Ufaransa kwa lengo la kusaidia kukarabati Lebanon.

Waziri Mkuu wa Lebanon, Fuad Siniora, anahudhuria kikao hicho.

Mapema Waziri Mkuu huyo alizungumzia umuhimu wa mkutano huo.

"Ninaamini hii ni fursa muhimu sana kwetu. Tunahitaji mkutano huu ili kupata msaada kutoka kwa nchi marafiki zetu.

Msaada tutakaoupata utalisaidia taifa letu kukabiliana na matatizo yalitokana na vita"

Kikao hicho kinalenga kusaidia ukarabati wa nchi hiyo iliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa wakati wa vita vya mwezi mmoja kati ya Hizbullah na Israil mwaka uliopita.

Umoja wa Ulaya tayari umeahidi kutoa msaada wa Euro milioni mia nne kwa miaka mitano ijayo.

Rais wa Ufaransa, Jacque Chirac pia ameahidi Ufaransa itaipa serikali ya Fuad Siniora mkopo wa Euro mia tano.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Bi Condoleezza Rice, ameahidi msaada wa ziada wa dola milioni mia saba na sabini.

Tangu mwezi Agosti, mwaka uliopita, Marekani imeipa Lebanon msaada wa dola zaidi ya bilioni moja.

Mgomo mkubwa uliotishwa na chama cha Hizbullah ulizitatiza shughuli nchini humo siku ya jumatatu iliyopita.

Watu watatu waliuawa na wengine kadhaa wakajeruhiwa kwenye makabiliano kati ya wafuasi wa chama cha Hizbullah na serikali.