1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa yuko pamoja na wahanga wa unyanyasaji kingono

Sekione Kitojo
17 Agosti 2018

Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis yuko katika upande wa wahanga wa zaidi ya mapadre 300 waliofanya unyama wa unyanyasaji  mkubwa kingono nchini Marekani wanaoshutumiwa kuwafanyia unyanyasaji zaidi ya watoto 1000.

https://p.dw.com/p/33IGU
Papst Franziskus
Picha: picture-alliance/dpa/S. Spaziani

Unyama  huo ulifanyika  katika  kiondi cha  miongo saba, yameeleza  makao  makuu  ya kanisa  Katoliki mjini  Vatican.

Wahanga  watambue kuwa  papa  yuko  upande wao, imesema  taarifa  ya  Vatican baada  ya  ripoti mbaya ya jopo la mahakama nchini  Marekani  kuchapishwa  siku  ya  Jumanne inayoelezea hatua za  kuficha madhila  hayo zilizofanywa  na  kanisa Katoliki. 

Bolivianer Toribio Ticona bei Kardinalsweihe im Vatikan
Makadinali wa kanisa KatolikiPicha: Reuters/T. Gentile

"Kuna  maneno  mawili yanayoweza  kueleza  hisia zinazokabili uhalifu  huu  wa  kutisha, aibu  na  masikitiko. Papa anachukulia  kwa dhati  kazi  ya  jopo  la  mahakama pamoja  na  ripoti iliyotoa. Papa analaani  bila kiasi unyanyasaji kingono watoto wadogo. Unyanyasaji ulioelezwa  katika  ripoti  ni  uhalifu  na kiroho ni wa kukemewa. Vitendo  hivyo  ni usaliti  wa  imani  ambayo  imewapora wale waliofanyiwa utu  wao na, pia imani  yao. Kanisa  linapaswa kujifunza  somo  gumu kutoka  yale  yaliyopita, na kunahitajika kuwajibika kwa  wale  waliofanya  vitendo  hivyo  na  wale  ambao waliruhusu  unyanyasaji  huo  kutokea."

Hayo  ni  maneno  katika  taarifa  ya   makao  makuu  ya  kanisa Katoliki  mjini  Vatican  iliyosomwa  na  msemaji  wa  kanisa  hilo Greg Burke.  "Wale ambao  wameathirika  ndio anaowapa  umuhimu wa  kwanza,  na  kanisa  linataka  kuwasilikiza ili  kuondoa maafa haya  ya  kutisha  ambayo  yanaharibu  maisha  ya  watu  wasio  na hatia,"  taarifa  ya  Vatican imesema.

Chile | Erzbischof Ricardo Ezzati
Kasisi Ricardo Ezzati akisimamia misa ya kwanza tangu kurejea kutoka Vatican mjini Santiago, baada ya makasisi wengi kujiuzulu kutokana na kashfa ya kuficha uhalifu wa kingonoPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Hildago

Ripoti  hiyo  inafikiriwa  kuwa  yenye ufafanuzi  mpana  zaidi  hadi sasa  kuhusiana  na  unyanyasaji  kingono  katika  kanisa  nchini Marekani, tangu  pale  Boston Globe  ilipofichua  kwa  mara  ya kwanza  kuwapo  kwa  mapadre wanaowalawiti  watoto  jimboni Massachusetts  mwaka  2002.

Lakini  wakati  ripoti  ya  Jumanne  imesababisha  kufikishwa mahakamani  mapadre  wawili, mmoja  wao  akiwa  amekiri  kuwa  na makosa, wengi  wa  wale  wanaohusika  wamekwisha  fariki  na uhalifu mkubwa  zaidi  ulitokea  muda  mrefu  sana  kuweza kuwafikisha  mahakamani  wahusika, maafisa  wamesema.

Uchunguzi  huo  wa  miaka  miwili  uliofanywa  na  jopo  la  wazee wa  baraza  la  mahakama  katika  dayosisi  zote  isipokuwa  mbili  tu katika  jimbo  la  Pennsylvania uliwaita  mashahidi  wengi  pamoja  na kurasa  karibu  nusu  milioni  cha  rekodi  za  kanisa  zilizokuwa  na "madai  mengi  dhidi  ya  zaidi  ya  mapadre  wahalifu 300."

Papst Franziskus
Papa Francis akisalimiana na waumini katika uwanja wa mtakatuifu Petro mjini VaticanPicha: Getty Images/A.Solaro

"Kiongozi  wa  kanisa  anatambua vizuri  ni  kiasi  gani  uhalifu  huu unaweza  kutikisa  imani  na  mioyo  ya  waumini na  kusisitiza  wito wa  kufanya  juhudi  kujenga  mazingira  salama kwa  watoto  na vijana  pamoja  na  watu  wazima  ambao kuna uwezekano wakarubuniwa. Wahanga  wafahamu  kwamba  Papa yuko  upande wao. Wale  walioathirika ni  muhimu  kwake  na  kanisa linataka kuwasilikiza ili  kuondoa maafa  haya  ya  kutisha  ambayo yanaharibu  maisha  ya  watu  wasio  na  hatia."

Zaidi  ya  wahanga  watoto 1,000  wametambuliwa, lakini  idadi halisi inaweza  kuwa  maelfu," jopo  hilo  limekadiria. Wahanga wamesababishiwa  hali  ya  fadhaa maishani, na  kujiingiza  katika madawa  ya  kulenywa, ulevi wa  kupindukia na  kutaka  kujiua, jopo hilo  limesema.

Mwandishi:  Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Josephat  Charo.