Papa mpya huyu hapa
13 Machi 2013Baba Mtakatifu Francisco wa Kwanza mwenye umri wa miaka 76 alichaguliwa hapo jana na makadinali 115 baada ya siku mbili ya uchaguzi na anamrithi Benedict wa kumi na sita mabaye alijiuzulu mwezi uliopita. Papa huyo ni wa 266 tangu kanisa hilo kuanzishwa miaka elfu mbili iliyopita na wa kwanza kuchaguliwa kutoka Amerika ya Kusini na wa kwanza kutotoka barani Ulaya tangu karne ya kumi na nane.
Franisco ni Jina kwanza kutumika
Jina lake Francisco pia ndiyo mara ya kwanza kutumika na papa. Amekuwa kadinali wa Argentina tangu mwaka 1988 na amekuwa ktaika mstari wa mbele katika usimamizi wa masuala ya kiutawala wa kanisa hilo na hivyo kudhihirisha kuwa ataweza kutekeleza majukumu ya kuwa papa vyema.
Mwaka 2005 inasemekana aliibuka wa pili kwa wingi wa kura baada ya Benedict wa 16. Papa Francisco wa kwanza amekuwa akijishughulisha sana kuwafunza na kuwalea makasisi katika eneo la Amerika ya kusini ambalo lina waumini wengi zaidi ya kote ulimwenguni na hilo kumfanya kuonekana kumweka katika hali nzuri kuongoza kanisa Katoliki, na amelibadili sura kanisa hilo katika eneo hilo la kihafidhina.
Aomba baraka za waumini
Katika hotuba yake ya kwanza katika ubaraza wa ghorofa ya Basilica aliwaomba waumini kote duniani wa nia na kheri njema wamuombee baraka na pia alimuombea Papa anayeondoka Benedikto wa Kumi na Sita.
Maelfu ya waumini tangu Jumanne wamekuwa wakikita kambi katika uwanja wa mtakatifu Petro wakisubiri kuuona moshi mweupe ukifuka kutoka paa la kanisa la Sisitine ambako Makadinali 115 walikuwa wamefungiwa hadi wampate papa mpya na baada ya kupiga kura mara tano,jana usiku saa moja,moshi mweupe ulionekana na kengele katika uwanja huo kupigwa huku waumini hao wakishangilia kwa vifijo na nderemo.
Wengi walitumai kuwa kwa mara ya kwanza papa mtakatifu atatokea katika eneo tofauti mbali na bara Ulaya huku kadinali kutoka Brazil Odilo Sherer na kadinali kutoka Ufilipino wakipigiwa upatu.
Mjini Buenos Aires kulijaa shangwe punde tu baada ya Papa Francisco wa kwanza kutangazwa kuwa papa mpya.Wengi walitumai kuwa kwa mara ya kwanza papa mtakatifu atatokea katika eneo tofauti mbali na bara Ulaya huku kadinali kutoka Brazil Odilo Sherer na kadinali kutoka Ufilipino wakipigiwa upato.
Papa Francisco wa kwanza anaelezwa kuwa atakabiliwa na kibarua kigumu cha kurejesha hadhi ya kanisa hilo ambayo imezongwa na kashfa za dhuluma za kingono,ufisadi na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe.
Mwandishi:Caro Robi/Afp/Dpa
Mhariri: Sudi Mnette