Pope : Mauaji ya Waarmenia ni mauaji ya kimbari
12 Aprili 2015Papa Francis amesema mwanzoni mwa misa maalum ya kumbukumbu katika kanisa la St.Basilica mjini Rome kwamba "Katika karne moja iliopita kizazi chetu cha binaadamu kimepitia maafa makubwa matatu yasio na kifani."
Misa hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kukumbuka mauaji makubwa ya Waarmenia yaliofanywa na vikosi vya Ottoman vya Uturuki ambayo yalianza mwaka 1915.
Amesema maafa ya kwanza ambayo yanahesabiwa kwa kiasi kikubwa kuwa ni mauaji ya kwanza ya kimbari ya karne 20 yaliwakumba Waarmenia,kanisa la Kikristo halikadhalika Wakristo wa madhehebu ya Katoliki na wale wa Othodoksi wa Syria,watu wa jamii ya Waasyria na Wachaldian ambao ni Wakristo wa asili huko Mashariki ya Kati na Wagiriki.
Francis amesema mauaji mengine mawili ya kimbari ya karne iliopita yalifanywa na Wanazi na utawala wa Stalin na kuongeza kwamba dunia hivi sasa iko katikati ya mauaji mengine ya kimbari ambako ni kukandamizwa kwa Wakristo Mashariki ya Kati.
Ukweli usiokanushika
Kiongozi wa Kanisa Katoliki la Armenia Askofu Mkuu Karenin wa Pili amemshukuru Papa mwishoni mwa misa hiyo iliojaa ufafanuzi na iliodumu kwa masaa mawili na nusu.
Kirill amesema "Mauaji ya Waarmenia ni ukweli wa kihistoria usiosahaulika na usiokanushika na uliota mizizi kwenye mikondo ya historia ya kisasa na uwelewa wa jumla wa wananchi wa Armenia. Kwa hiyo jaribio lolote lile la kuyafuta mauaji hayo kwenye historia na kutoka kwenye kumbukumbu yetu ya pamoja litashindwa."
Wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia takriban watu milioni 1.5 inakadiriwa waliuwawa katika ardhi ya Ottoman katika matukio ambayo yanatambuliwa na mataifa mengi kuwa ni mauaji ya kimbari lakini sio Uturuki taifa lililokuja kurithi nafasi ya Falme ya Ottoman.
Kumbukumbu rasmi za mauaji hayo ya kimbari ya mwaka 1915-1916 zimepangwa kuanza Aprili 24 nchini Armenia.
Papa pia amesema katika ujumbe wa maandishi uliowasilishwa kwa viongozi wa kidini na wa kisiasa wa Armenia baada ya misa hiyo kwamba sio tu wajibu wa wananchi wa Armenia na Kanisa duniani kukumbuka yote yale yaliyotokea bali ni wajibu wa kizazi kizima cha binaadamu.Halikadhalika ameziombea Armenia na Uturuki zipatane.
Tamko la mauaji ya kimbari sio la kwanza
Hii sio mara ya kwanza kwamba Makao Makuu ya Kanisa Katoliki duniani Vatican kutumia neno "mauaji ya kimbari" kuyaelezea matukio hayo yaliyotokea miaka 100 iliopita.
Papa amekariri tangazo la pamoja la mwaka 2000 kutoka kwa mtangulizi wake Mtakatifu John Paull wa Pili na Karekin wa Pili. Papa Francis alitumia maelezo hayo hayo katika mkutano wa mwezi wa Juni 2013 na wawakilishi wa Armenia huko Vatican.
Wakati huo wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilishutumu matamshi ya Papa kuwa "hayakubaliki" na kuyaonya makao makuu hayo ya Kanisa Katoliki dhidi ya kuchukuwa hatua ambazo zinaweza kusababisha madhara yasiorekebishika katika uhusiano wao.
Wizara hiyo ilisema kile kinachotarajiwa kutoka kwa papa kutumia wajibu wake wa ofisi ya kidini katika kuchangia kuleta amani duniani badala ya kukuza uhasama kutokana na masuala ya matukio ya kihistoria.
Uturuki yakanusha mauaji ya kimbari
Uturuki ambayo ni nchi ya Kiislamu inakubali kwamba Wakristo wengi wa Armenia waliuwawa katika mapigano yaliyoanza mwaka 1915 lakini inakanusha kwamba mamia kwa maelfuya watu waliuwawa katika mapigano hayo kustahiki kuitwa mauaji ya kimbari.
Armenia yenyewe na baadhi ya wanahistoria na mabunge ya nchi za kigeni wanayataja mauaji hayo ya Waarmenia yaliyotokea karne moja iliopita kuwa ni " mauaji ya kimbari"
Lakini Marekani na washirika wengine wa Uturuki
wanajiepusha kutumia neno hilo kwa kuchelea kuharibu uhusiano na serikali ya Uturuki ambayo ni mshirika muhimu wa kimkakati huko Mashariki ya Kati.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa
Mwandishi : Caro Robi