Papa: Mapadri wanatakiwa kuwa karibu na waumini
29 Machi 2018Papa Francis ametoa ujumbe huo wa Alhamisi Kuu wakati wa Ibada ya kubariki mafuta ya Krisma ambayo ni maalum kwa ajili ya kuonyesha umoja wa Kanisa Katoliki wakati wa kipindi cha kuelekea kuadhimisha sikukuu ya Pasaka. Katika mahubiri yake Papa amewasihi mapadri kuwa karibu na watu muda wote.
Amesema hata wakati watu wanapotenda dhambi ya uzinzi, mapadri hawapaswi kuwahukumu kwa kuzingatia sheria za Kanisa, na badala yake wawasaidie kuwaonyesha njia sahihi kwa kuwahubiria mara kwa mara wajiepushe na dhambi.
''Tangu sasa usifanye dhambi tena. Tuwaambie kwa sauti ya upole na unyenyekevu, hali itakayomfanya mtu mwenye dhambi ajitafakari na kutubu,'' alisema Papa Francis.
Papa ameutoa ushauri huo wakati ambapo wahafidhina wa Kanisa Katoliki wametoa malalamiko kwamba kiongozi huyo analigawa kanisa kutokana na kuwaruhusu Wakatoliki waliotengana au waliofunga ndoa kwa mara nyingine kupokea Sakramenti.
Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na mapadri kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Papa Francis amesema Yesu hakuipuuza sheria katika hadithi ya kwenye Biblia wakati alipokataa kumhukumu mwanamke mzinzi.
Aidha, Papa amesema hakuna jehanamu ambayo roho za watu wenye dhambi zinateseka milele. Amesema baada ya kifo, roho za watu waliotubu zinasamehewa na Mungu na kujiunga na tafakari yake, lakini wale wasiotubu, hawawezi kusamehewa na watapotea. Hivyo kinachobakia ni kupotea kwa roho yenye dhambi.
Ibada ya kubariki mafuta ya Krisma ni moja kati ya ibada mbili za misa ambazo huadhimishwa siku ya Alhamisi Kuu, siku nne kabla ya Jumapili ya Pasaka, ikiwemo misa ya jioni ambapo anawaosha miguu watu 12. Tukio hilo linafanyika jioni hii katika gereza la Regina Coeli na linawajumuisha Wakatoliki, Waislamu, Waorthodox na muumini mmoja wa madhehebu ya Buddha.
Alhamisi Kuu ni siku ambayo Wakatoliki wanaamini kuwa Yesu alianzisha ukuhani wakati wa karamu ya mwisho na wafuasi wake kabla ya kusalitiwa na kukamatwa.
Kesho Ijumaa, Papa Francis ataongoza Njia ya Msalaba na ibada ya misa ya Ijumaa Kuu kukumbuka mateso ya Yesu. Usiku wa Jumamosi ataadhimisha misa ya kesha la Pasaka katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na Jumapili ataongoza misa ya Jumapili ya Pasaka.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, AFP
Mhariri: Saumu Yusuf