1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis atoa waraka kuhusu familia

Grace Kabogo8 Aprili 2016

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amesema dhamira ya mtu inapaswa kuelezea mitazamo ya waumini wa Kikatoliki kuliko kuangalia zaidi sheria za Vatican kuhusu upendo, ngono, ndoa na masuala ya familia.

https://p.dw.com/p/1ISA8
Papa Francis
Picha: picture-alliance/S. Spaziani

Hayo yamo katika mwongozo mpya wa Kanisa uliopewa jina 'Furaha ya Upendo' au 'Amoris Laetitia' kwa lugha ya Kilatini, ambao umetangazwa leo na Papa Francis mjini Vatican. Mwongozo huo ambao uko kwenye waraka wenye kurasa 260, hata hivyo haujayafanyia mabadiliko yoyote yale mafundisho ya kanisa.

Mwongozo huo uliosubiriwa kwa hamu na muda mrefu, huenda ukawakasirisha watetezi wa mabadiliko makubwa katika Kanisa, kutokana na hatua ya Papa Francis kutangaza kuwa ndoa ya jinsia moja sio ndoa sawa na ile ya mume na mke. Amesema Kanisa linapinga hatua ya kuutambua uhusiano wa jinsia moja.

Papa amebainisha kuwa maaskofu ambao walipitia mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu ndoa za jinsia moja katika sinodi za mwaka 2014 na 2015, wamegundua kwamba hakuna mazingira yoyote yanayozingatia ndoa za mashoga kuwa katika njia sawa na mpango wa Mungu kwa ajili ya ndoa na familia.

Papa Francis amesema dhamira ya mtu binafsi ya Wakatoliki ndiyo itamuongoza kuhusu upendo na familia na hiyo sio kazi ya Vatican kuanisha kuhusu suala hilo. Amesema Kanisa limekuwa likijihami sana katika siku za nyuma kwa kung'ang'ania mtazamo uliojengeka kuhusu ndoa na kwamba Vatican ilihitaji kujikosoa kuhusu suala hilo.

Kanisa Katoliki halijabadilisha mafunzo yake kuhusu familia
Kanisa Katoliki halijabadilisha mafunzo yake kuhusu familiaPicha: Colourbox

Kanisa lilihitaji kujikosoa

Kulingana na mwongozo huo, wanandoa wa Kikatoliki waliopeana talaka na waumini wanaoishi pamoja bila ya kufunga ndoa, wanapaswa kukaribishwa na kupewa mwongozo. Padri Joseph Mosha kutoka Vatican anasema mwongozo huo utasaidia kutoa mwanga kwa familia na waumini wanapaswa kuelewa kwamba mafundisho ya Kanisa yamewekwa wazi mbele yao.

Kauli hiyo ya Papa imeugeuza mtazamo wa jadi kuhusu watu wanaoishi bila kufunga ndoa, ambao ilichukuliwa kama wanaishi katika dhambi. Hata hivyo, hakuweka wazi iwapo Wakatoliki ambao wanaishi bila ndoa na wale waliotalakiana, wanaweza kupokea Sakramenti wakati wa Ibada ya Misa. Papa Francis pia ametoa wito wa kuondolewa kwa kila ishara ya ubaguzi usio wa haki dhidi ya watu binafsi kuelekea mrengo wa jinsia.

Mwongozo huo umeacha wazi kwa maaskofu katika kila nchi kufafanua mafundisho ya Kanisa Katoliki kuambatana na utamaduni wa maeneo husika. Aidha, Papa Francis amewahimiza mapadri kutumia hekima na busara wakati wanapozishughulikia familia zilizoumizwa pamoja na kuwa na huruma badala ya kutoa hukumu haraka.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,AP

Mhariri: Iddi Ssessanga