Papa Francis atimiza umri wa miaka 80
17 Desemba 2016Ikiwa ni miaka mitatu na miezi tisa baada ya kuchaguliwa kwake, Papa Francis ambaye ni wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini bila kuchoka na kwa kasi ileile ameendelea kukaribia hatua ambayo itahusisha makadinali kufanya kazi kwa muda kutokana na hali zao ama kiafya au umri.
Lakini pia hajaonyesha uwezekano wa kufuata hatua ya kihistoria ya mtangulizi wake Papa Benedict wa 16 aliyestaafu kutokana na kuchoka mnamo mwaka 2013. Hadi sasa na hakuna kiashiria kwamba hilo linaweza kutokea hivi karibuni.
Kama ilivyo kila wakati kwenye uongozi wake, Jumamosi hii pia itakuwa ni siku yake ya kufanya kazi kwa kiongozi huyo asiyeendekeza siku za mapumziko. Atashiriki ibada ya asubuhi pamoja na makadinali wengine, na kufuatiwa na mikutano kati yake na Rais wa Malta na afisa wa ngazi za juu wa Vatican.
Haya yatakuwa ni maadhimisho yake ya nne kwa askofu huyo wa zamani wa Buenos Aires ambayo amesherehekea katika nyumba ya Mtakatifu Martha, ambayo ameifanya makao yake ndani ya Vatican. Wakristo Bilioni 1.2 duniani, wamekwishazoea kumuona Papa katika maeneo mbalimbali duniani.
Zipo dalili zinazoonyesha kwamba anachoka, ni dalili za kawaida kwa mwanadamu aliyefikia umri kama wake ambaye alishapoteza figo moja wakati wa ujana wake na mara nyingine huonekana akikunja uso kutokana na maumivu anayoambatana nayo.
Mara nyingine Papa Francis huonekana akibadilika, na hiyo huonyesha kwamba anazungumzia kitu kizito na muhimu kilichopo moyoni mwake. Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na kuzama kwa wahamiaji wanaokimbilia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterrania, unyanyasaji wa masikini ama suala la hivi karibuni la kuvunjwa kwa nguvu za kilimo cha biashara.
Alizaliwa kwenye familia yenye turathi ya Italia, Desemba 16, 1936, Jorge Bergoglio ambalo ndio jina lake halisi alikuwa Papa wa 266 baada ya kuchaguliwa kwake mwezi Machi mwaka 2013.
Tokea mwanzo alionekana kuwa ni mtu mwenye haraka. Mara kadhaa alijiona kama hafikirii kuwa hapo kwa muda mrefu. Alisema, "Ninataka kanisa masikini kuwa ni la watu masikini”. Na kwa mapana zaidi, nia yake ilikuwa ni kulibadilisha kanisa na kuwa taasisi ya huruma, ambayo itaweza kuwasaidia waumini katika matatizo yao ya kila siku.
Kwenye Jubilei yake ya kwanza, Papa Francis aliutoa mwaka huo kwa ajili ya huruma. Yeye alinaamini hilo ni suala muhimu zaidi katika kazi ya kanisa, badala ya kuangazia laana na hukumu.
Huku akikabiliwa na upinzani mkali kwenye uongozi wake na hususan kutoka nchi zinazoendelea, Francis amefanikiwa kwa kiasi kidogo katika mikakati yake ya kubadilisha mafundisho ya kanisa Katoliki.
Katika kurejelea masuala yaliyosumbua kanisa ambayo ni pamoja na kuishi pamoja na misimamo kuhusu mapenzi ya jinsia moja ama talaka ndani ya kanisa, hayakupata suluhu ya pamoja, hali iliyowaudhi wahafidhina na kuwakatisha tamaa wenye misimamo mikali.
„Mimi ni nani hata nihukumu?" Papa Francis aliwahi kuuliza wakati alipoulizwa maoni yake kuhusu mapenzi ya jinsia moja, ambayo yamechukuliwa kama ugonjwa kwenye kanisa Katoliki.
Na kuhusu kuwezesha wanawake kuhudumu kama mashemasi kama hatua za mwanzoni za Ukristo, baadhi wanaona kama Papa Francis amefungua milango ya kuwawezesha wanawake kuwa mapadri. Kwake, kanisa ni kama hospitali na si kizuizi cha mteja, amesema mtaalamu wa Vatican, Marco Politi. Lakini hajagusa mafundisho. Kwa maana hiyo hajafika mbali.
Lakini mmoja wa watazamaji kutoka Vatican, Marco Tosatti anasema, „Papa Francis ameleta mkanganyiko mkubwa ndani ya kanisa”. Ni Papa wa waandishi wa habari, amelipa kanisa mtizamo mwepesi na wa kirafiki.
Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Grace Patricia Kabogo