1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Papa Francis aongoza mazishi ya Papa Mstaafu Benedict XVI

5 Januari 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameongoza Ibada ya mazishi ya Papa Mstaafu Benedict XVI katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

https://p.dw.com/p/4Ll5i
BG - Beisetzung Papst Benedikt
Picha: GUGLIELMO MANGIAPANE/REUTERS

Kwa mara ya kwanza katika historia ya sasa, papa aliyeko madarakani ndiyo ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na kuhubiri katika mazishi ya mtangulizi wake. Maelfu ya waombolezaji wamejitokeza mapema Alhamisi asubuhi katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kuhudhuria mazishi ya mwanateolojia huyo wa Ujerumani.

Soma zaidi: Maisha ya Papa Mstaafu Benedict XVI

Kengele ziligongwa na umati wa watu ulipiga makofi wakati ambapo jeneza lenye mwili wa Benedict likipitishwa kutoka sehemu lililpokuwa limewekwa ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na kulihamishia mbele ya altare iliyo mbele ya viwanja hivyo, huku makadinali waliovalia mavazi mekundu wakitazama.

Papa Mstaafu Benedict XVI, hakuwa tena kiongozi wa taifa, lakini viongozi mbalimbali duniani, akiwemo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, wamehudhuria mazishi yake. Vatican ilizialika rasmi nchi za Italia na Ujerumani pekee kuhudhuria mazishi hayo, na kuzishauri balozi za kigeni kwamba viongozi wengine wowote wanaotaka kuhudhuria, wanaweza kufanya hivyo lakini kwa ''uwezo wao binafsi.''

BG - Beisetzung Papst Benedikt
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis akiongoza Ibada ya mazishi ya Papa Mstaafu Benedict XVIPicha: GUGLIELMO MANGIAPANE/REUTERS

Kwa mujibu wa Vatican, viongozi wengine waliohudhuria ni Rais wa Poland Andrzej Duda, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Czech Petr Fiala na Rais wa Slovenia Natasa Pirc Musar. Malkia Sofia wa Uhispania na Mfalme Philippe na Malkia Mathilde wa Ubelgiji pia wanahudhuria.

Nchi nyingi zimewakilishwa na mabalozi wao katika makao makuu ya Kanisa Katoliki huko Vatican. Zaidi ya makardinali 4,000, mapadri na maaskofu wanahudhuria mazishi hayo.

Kanisa limepoteza mtu muhimu

Aliyekuwa rais wa baraza la kipapa la kuimarisha umoja wa Kikristo, Mwadhama Walter Kardinali Kasper, amesema kanisa limempoteza mtu muhimu sana. ''Tumempoteza mtu muhimu sana ambaye pia ameacha alama muhimu katika historia ya Kanisa katoliki, kwanza kutokana na tabia yake, fadhili na tabasamu, lakini pia maandiko yake ya teolojia na kiroho,'' alisema Kasper.

Kwa mujibu wa taarifa za awali za Vatican, mazishi ya Benedict hayatokuwa na shughuli kubwa sana, kwa lengo la kuenzi matakwa yake, ya kuwa na mazishi ya kawaida.

BG - Beisetzung Papst Benedikt
Makardinali katika ibada ya mazishi ya Papa Mstaafu Benedict XVIPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Mwili wa Benedict utazikwa katika kaburi ambalo mwili wa Papa John Paul II ulizikwa kabla ya kuhamishwa kwa ajili ya kutangazwa kuwa Mwenye Heri mwaka 2011. Makaburi hayo ya kipapa yako chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mnamo mwaka 2014 alitangazwa kuwa Mtakatifu.

Maombolezo nchi mbalimbali

Ureno imeitangaza Alhamisi kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa, huku nchini Italia bendera zikipepea nusu mlingoti katika majengo yote ya umma. Nchini Ujerumani kengele kwenye makanisa yote ziligongwa majira saa tano kamili asubuhi kwa ajili ya kumbukumbu ya papa wa kwanza Mjerumani katika kipindi cha miaka 1,000 iliyopita.

Kwa mujibu wa Vatican, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 195,000 tayari wametoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Benedict katika siku tatu zilizopita. Papa Benedict alikuwa ni papa wa kwanza wa Kanisa Katoliki katika kipindi cha miaka 600 kujiuzulu wadhifa wake kabla ya kufariki.

(AP, AFP, DPA, Reuters)