1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aomba amani ulimwenguni

21 Aprili 2014

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis katika hotuba yake ya Pasaka Jumapili (20.04.2014) ameshutumu matumizi ya ovyo wakati watu wakikabiliwa na njaa na kutaka kukomeshwa kwa mizozo Syria,Ukraine na Afrika

https://p.dw.com/p/1BlQG
Papa Francis akiupungia umati kabla ya kuwasilisha ujumbe wake wa "Urbi et Orbi" katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican.(20.04.2014)
Papa Francis akiupungia umati kabla ya kuwasilisha ujumbe wake wa "Urbi et Orbi" katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican.(20.04.2014)Picha: Reuters

"Tunakuomba wewe Bwana Yesu, kukomesha vita vyote na kila mzozo,uwe mkubwa au mdogo wa kale au wa karibuni" amesema hayo katika ujumbe wake wa "Urbi et Orbi" unaomaanisha kwa"Mji na Dunia".

Francis akiadhimisha Pasaka ya pili akiwa kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ameendesha misa kwa umati wa watu unaofikia 150,000 waliofurika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Peter na kupindukia uwanja huo.

Akizungumza chini ya mbingu an'gavu kufuatia mvua za usiku zilizorowesha maelfu kwa maelfu ya mauwa yalioupamba uwanja huo, ujumbe wa Papa Francis ulijikita juu ya kuteseka kwa watu duniani kote.

Ameomba Mungu kwa kusema "tusaidie kuondokana na janga la njaa linalozidi kuchochewa na mizozo na matumizi makubwa ya ovyo ambayo kwayo mara nyingi tunahusika nayo."

Mtetezi wa maskini

Tokea kuchaguliwa kwake akiwa papa wa kwanza asiyetoka Ulaya katika kipindi cha miaka 1,300, Francis amewatetea maskini ambao wamekuwa alama yake katika wadhifa wake huo,mara nyingi akishutumu mataifa ya yalioendelea na tabia ya ubepari na kuendekeza matumizi makubwa yasiokuwa na maana.

Papa Francis akiupungia umati kabla ya kuwasilisha ujumbe wake wa "Urbi et Orbi" katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican.(20.04.2014)
Papa Francis akiupungia umati kabla ya kuwasilisha ujumbe wake wa "Urbi et Orbi" katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican.(20.04.2014)Picha: Reuters

Papa huyo mwenye umri wa miaka 77 akivalia mavazi meupe kwa ajili ya misa hiyo, amewaombea watu walioko katika jamii ambao ni rahisi kuathirika kwa unyonyaji, dhuluma na kutelekezwa kwa watoto,wanawake,wazee na wahamiaji.

Pasaka ni siku muhimu sana katika kalenda ya Ushirika Mtakatifu kwa sababu inaadhimisha siku ambayo Wakristo wanaamini Yesu alifufuka baada ya kusulubiwa kwake na Kanisa inaiona siku hii kuwa ni alama ya matumaini, amani na upatanishi miongoni mwa watu na mataifa.

Mazungumzo ya amani ya ujasiri

Papa ameitaka jumuiya ya kimataifa kutumia ujasiri katika mazungumzo ya kutafuta amani ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na kuchelewa mno kupatikana nchini Syria ambapo zaidi ya watu 150,000 wameuwawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe,theluthi moja kati yao wakiwa ni raia. Mamilioni ya watu wameikimbia nchi hiyo.

Papa Francis akiongoza Misa ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican. (20.04.2014)
Papa Francis akiongoza Misa ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican. (20.04.2014)Picha: Reuters

Amesema " Hususan tunaiombea Syria kwamba wale wote wanaoteseka na athari za mzozo huo waweze kupokea msaada wa kibinaadamu unaohitajika na kwamba pande zote mbili hazitotumia tena kamwe nguvu zinazosababisha maafa hususan dhidi ya raia wasiokuwa na hatia"

Papa Francis amemuomba Mungu azitie mwanga na msukumo juhudi za kuendeleza amani Ukraine ili kwamba wale wote wanaohusika kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa wafanye kila juhudi za kuzuwiya matumizi ya nguvu na kwa roho ya umoja na mazungumzo watafute njia ya kujenga mustakbali wa nchi hiyo.

Pia ametaka kukomeshwa kwa umwagaji damu na matumizi ya nguvu nchini Iraq,Venezuela, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wagonjwa hawakusahauliwa

Papa Francis pia ametowa wito wa kuwekewa nadhari zaidi wahanga wa gonjwa thakili linalosababisha vifo la Ebola huko Guinea Conakry,Sierra Leone na Liberia na kuwahudumia wale wanaoteseka na magonjwa mengine mengi yanayoenea kutokana na kupuuzwa na umaskini uliokithiri.

Papa Francis akiongoza Misa ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican. (20.04.2014)
Papa Francis akiongoza Misa ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican. (20.04.2014)Picha: Reuters

Papa ametaka kukomeshwa kwa mashambulizi ya kinyama ya kigaidi nchini Nigeria kwa kile kinachonekana kuwa alikuwa akilikusudia kundi la itikadi kali za Kiislamu la Boko Haram ambalo mapema mwezi huu liliwateka nyara wasichana 130 kutoka shule moja kaskazini mwa nchi hiyo.

Ibada za Pasaka ya Jumapili ni hitimisho la siku nne za harakati za Wiki Takatifu kwa papa huyo.Jumapili ijayo atawatangaza kuwa watakatifu kwa wakati mmoja Papa John Paul wa Pili aliyeongoza Kanisa Katoliki kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 2005 na Papa John wa ishrini na tatu aliekuwa papa kuanzia mwaka 1958 hadi mwaka 1963.

Mamilioni ya watu wanatazamiwa kumiminika Rome kwa ajili ya tukio hilo ambapo kwa mara ya kwanza papa wawili wanatangazwa kuwa watakatifu kwa wakati mmoja na mara ya kwanza kutangazwa kwa utakatifu wa papa tokea mwaka 1954.

Mwandishi : Mohamed Dahman / Reuters/dpa

Mhariri : Bruce Amani