Papa Francis akutana na wahanga wa vita vya Kongo
2 Februari 2023Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameelezea masikitiko yake na kuwapa pole wahanga wa ghasia za kikatili katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Masikitiko hayo ameyatoa jana jioni wakati alipokutana na wahanga wa vita na machafuko ya kisiasa kutoka mashariki mwa Kongo ambao walielezea ukatili waliopitia.
Akizungumza kwa hisia baada ya kukutana na wahanga hao kwenye ubalozi wa Vatican mjini Kinshasa, Papa Francis amesema yuko karibu na waathirika hao na amelaani vikali vita pamoja na mauaji ya kinyama.
Amesema maumivu yao ni yake pia, na kwamba ujumbe huo anautoa kwa wote waliopitia unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji, vijiji vyao kuchomwa moto na walioporwa mazao na mifugo yao. Papa amesema vita vya Kongo vimesababisha uvunjwaji wa haki za binadamu, na hivyo kuacha madonda ambayo ni vigumu kuweza kupona.