Papa Francis akemea matumizi ya anasa
25 Desemba 2015
Baba Mtakatifu, kupitia hotuba yake ya kila mwaka ya Misa ya Mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewataka Wakristo kila mahali kupunguza mambo mengi ya jamii ya kisasa, ambayo amesema "imechafuliwa sana na tamaa ya ulaji na raha, kupenda mali na ubadhirifu, mwonekano na kujipenda kupita kiasi."
Ukristo unawataka waumini "kutenda wakiwa na akili timamu, kwa maneno mengine wakiwa wepesi, wenye mizania, wenye uwezo wa kuona na kufanya yaliyo muhimu," alisema papa huyo mwenye umri wa miaka 79, kiongozi wa Wakatoliki bilioni 1.2 duniani.
Katika baadhi ya nchi duniani, Wakristo waliiadhimisha siku hii wakiwa na wasiwasi wa maisha yao, na wengine hata kupigwa marufuku kuisherehekea, jambo ambalo Papa Francis alilitolea kauli kwa kusema "tunahitaji kuwa na mfumo madhubuti wa haki, kujiweza na kutenda mapenzi ya Mungu."
Akikemea kile alichokiita "utamaduni wa uhasama ambao mara zote hugeuka balaa", papa huyo mwenye asili ya Argentina aliwataka Wakatoliki kuchanganya sala na tabia ya "kujiamini, busara na rehema" baada ya mwaka mzima wa machafuko ya kilimwengu ambao ulishuhudia wakimbizi na wahamiaji milioni moja, wengi wao kutoka Syria, wakiingia Ulaya kusaka maisha bora zaidi.
Huku kukiwa na kiwango kikubwa cha walinda usalama kisicho cha kawaida kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro, kiongozi huyo aliyeonekana kushawijika kutokana na kuugua mafua, alipaza sauti yake kuwataka waumini walio kwenye mazingira magumu kukabiliana na khofu walizonazo.
Krismasi Bethlehem
Mjini Bethlehem ulio katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, kiongozi wa Kanisa la Katoliki katika Ardhi Takatifu Fouad Twal alihudhuria misa ya kitamaduni ya usiku wa manane katika kanisa lililojengwa katika mahala ambapo Wakristo wanaamini ndipo alipozaliwa Yesu miaka 2,015 iliyopita. Askofu Twal anayeishi Jerusalem alipaswa kuvuuka ukuta uliojengwa na Israel kuitenganisha miji hiyo miwili, huku akihubiri ujumbe wa amani na upendo.
Hata hivyo, kinyume na miaka iliyopita, sherehe za mwaka huu hazikuwa na shamra shamra nyingi kufuatia kuzuka kwa ghasia mjini Jerusalem na maeneo ya Wapalestina. Ghasia hizo zimepunguza sana idadi ya mahujaji wanaoutembelea mji wa Bethlehem na Ardhi Takatifu ya Jerusalem, na ni idadi ndogo tu ya watu waliojitokesha kwenye ibada iliyoongozwa na na Askofu Twal.
Maandamano ya mitaani na mashambulizi baina ya Wapalestina na Waisraeli yaliyoanza mwezi Oktoba, yamepelekea vifo vya Wapalestina zaidi ya 130, Waisraeli 19, Mmarekani mmoja na Mueritrea mmoja. Israel inasema Wapalestina wengi waliouawa walikuwa washambuliaji, huku wengine wakiuwa kwenye makabiliano.
Ibada ya mwaka huu kwenye mji wa Bethlehem, eneo linaloamika kuzaliwa Yesu ni maalum kwa wahanga wa ghasia hizo na familia zao, alisema Askofu Twal akiongeza kwamba sherehe "zitakuwa za kawaida kutokana na ghasia kwenye maeneo ya Wapalestina, Israel na duniani kote."
Askofu huyo pia aliwatolea wito wachungaji kuzima taa za miti ya Krismasi kwa dakika tano kuonesha mshikamano wao na wahanga wa ghasia na ugaidi. Taa kwenye miti ya Uwanja wa Manger zilizimwa kwa dakika chache saa 1:00 magharibi.
Khofu msimu wa Krismasi duniani
Majaaliwa ya Wakristo katika eneo la Mashariki ya Kati, hasa kule ambako wamekuwa wakitishiwa na kusonga mbele kwa magaidi wa kundi la Dola la Kiislamu, yalipewa nafasi sana mwaka huu.
"Tunaomba kwa ajili ya kurejea kwa amani na usalama na kurejea kwa wakimbizi nchini kwao," alisema Farida, mmoja wa waumini wa Kikristo alipokuwa akiwasilik kwenye Kanisa la Uokovu la Mama Maria mjini Baghdad, Iraq.
Alisema jamaa zake 12 waliuawa wakati kundi la Dola la Kiislamu lilipouchukuwa mji wa pili kwa ukubwa, Mosul, mwaka 2014 na kuwaamuru Wakristo kusilimu, kulipa kodi kubwa kama raia wa daraja la pili au kuuawa.
Nchini Somalia, serikali imepiga marufuku sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya kwenye taifa hilo lenye Waislamu wengi, ikisema sherehe kama hizo zitawavutia washambuliaji wa siasa kali za kidini.
Hali kama hiyo pia imetokea kwenye nchi tajiri kwa mafuta, Brunei, ambako serikali imetishia kifungo cha miaka mitano kwa wale watakaokaidi marufuku ya "sherehe za wazi na za kupindukia."
Na katika maeneo yenye matatizo kusini mwa Ufilipino, wakulima saba wa Kikristo waliuawa baada ya wapiganaji wa msituni wa Kiislamu kufanya mashambulizi kadhaa huko.
Wakati huo huo, balozi za Marekani na Uingereza nchini China zilitoa onyo lisilo la kawaida juu ya uwezekano wa mashambulizi dhidi ya raia wa Magharibi katika kiunga kimoja mashuhuri za mji wa Beijing wakati wa sikukuu ya Krismasi.
Nchini Ufaransa, hatua za usalama zimeimarishwa kwenye makanisa kufuatia mashambulizi ya mwezi uliopita ambapo watu 130 waliuawa mjini Paris.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Bruce Amani