Papa Francis aitetea kauli yake
1 Mei 2017Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametetea kauli yake aliyoitoa kwamba vituo vya wakimbizi ambako wanawekwa wahamiaji wanaoingia barani Ulaya, havina tofauti na ''Kambi za Mateso''.
Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege wakati anarejea Roma kutoka Misri, Papa Francis amesema haelewi kwa nini kauli yake imezua utata, kwa sababu ni kweli katika baadhi ya vituo wakimbizi wanarundikwa na kisha wanazuiwa kuondoka, hivyo kambi hizo hazina tofauti na kambi za mateso.
Asema hakukosea
Papa amesema sio kwamba aliteleza ulimi wakati alipotoa matamshi hayo, hakukosea na alimaanisha alichokisema, kwani watu wengi wanafungwa katika kambi hizo na hawawezi kufanya lolote. Mnamo Aprili 22 mwaka huu, akiwa katika kisiwa cha Tiber mjini Roma, Papa Francis anayejulikana kwa misimamo yake ya kupinga ukatili, alisema kuwa kambi nyingi za wakimbizi ni sawa na kambi za mateso kutokana na kufurika kupita kiasi.
''Hizi kambi za wakimbizi ni sawa na kambi za mateso. Nyingine ziko Italia, na sehemu nyingine, nchini Ujerumani sina uhakika. Wafikirie wale watu ambao wanafungwa kwenye kambi na hawawezi kwenda nje. Fikiria kile kilichotokea Ulaya kaskazini wakati walipotaka kuvuka bahari kwenda England, lakini walifungiwa ndani,'' alisema Papa.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani alizitaka serikali kuwaachia wakimbizi na wahamiaji watoke nje ya vituo wanavyoshikiliwa. Baada ya kuzuru kisiwa cha Tiber, Papa Francis pia alikutana na wahamiaji katika Kanisa Kuu la Roma, na kuwaelezea ziara yake aliyoifanya katika kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki mwaka uliopita.
Hata hivyo, Baba Mtakatifu alizipongeza nchi zinazowasaidia wakimbizi na kuzishukuru kwa kukabiliana na mzigo huo mkubwa wa ziada, kwa sababu inaonekana kama mikataba ya kimataifa ni muhimu zaidi kuliko haki za binaadamu. Lakini hakuelezea zaidi kuhusu mikataba hiyo, ingawa inaonekana alikuwa akizungumzia makubaliano yanayowazuia wakimbizi kuvuka mipaka, kama vile mkataba kati ya Umoja wa Ulaya na Libya na Umoja wa Ulaya na Uturuki.
Mitazamo tofauti ya jamii za Wayahudi
Wakati huo huo, baadhi ya jamii za Wayahudi zimeikosoa vikali kauli hiyo, huku jamii nyingine za Kiyahudi zikisema kuwa ni halali. Jumuiya ya Wayahudi nchini Marekani, AJC imeikosoa vikali kauli ya Papa Francis na imemtaka aangalie upya matumizi ya matamshi yake.
Mkuu wa AJC, David Harris amesema mazingira ambayo wakimbizi wanaishi kwa sasa kwenye baadhi ya nchi za Ulaya, kweli huenda yakawa magumu na kuhitaji uangalizi wa jumuia ya kimataifa, lakini hayako sawa na kambi za mateso.
Ama kwa upande mwingine, Kamati ya Kimataifa ya kambi ya mateso ya Auschwitz, IAC, imesema matamshi ya Papa Francis ni halali.
Akizungumza mjini Berlin, Ujerumani Makamu wa Rais wa kamati hiyo iliyoanzishwa na manusura wa kambi ya maangamizi ya Auschwitz, Christoph Heubner, amesema Papa ametoa kauli hiyo kwa nia njema na haioni kama ni ya kikatili.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga