Papa Francis aomba radhi kwa yaliyokea
16 Februari 2016Katika wakati ambapo jimbo la Chiapas linasemekana kuwa jimbo lenye waumini wachache wa kikristo,maelfu ya watu walimiminika katika uwanja wa michezo kusikiliza misa ambayo kwa mara ya kwanza kabisa imefanyika kwa lugha za wenyeji wa eneo hilo- Maya. Binafsi Papa Francis alitamka maneno machache kwa mojawapo wa lugha hizo za kienyeji na kunukuu Maandishi ya kale wa jamii ya Maya-Popol Vuh."Mara kadhaa,na kwa utaratibu ulioandaliwa makusudi,jamii yenu watu hawakuwa wakiielewa na kuamua kuitenga,amesema Papa huyo,mwenye umri wa miaka 79 mzaliwa wa Argentina,alieomba samahani kwa kile alichokitaja kudharauliwa maadili yao,utamaduni na mila zao na wale waliolewa madaraka,fedha na soko na kuwapokonya ardhi zao."
Papa Francis aeneza nasaha dhidi ya uhalifu na rushwa
Takriban asili mia 30 ya wakaazi wa Chiapas hawazungumzi kihispania,lugha ya watawala wa kikoloni walioiteka nchi hiyo katika karne ya 16,wakawadhulumu wakaazi asilia na kuwashawishi wajiunge na dini ya kikristo.
Papa Francis ameshawahi kuomba radhi mwaka jana alipoitembelea Bolivia pia kwa makosa yaliyofanywa na kanisa katika enzi za ukoloni.
Katika wakati ambapo Mexico ni nchi ya pili yenye waumini wengi zaidi wa kikatoliki ulimwenguni,baada ya Brazil,asili mia 82 ya wakaazi wake milioni 122 wanajitambulisha na imani hiyo,katika jimbo la Chiapas wanaojitambulisha na Vatican hiyo idadi yao ni asili mia 58 tu.
Papa Francis anaitumia ziara yake ya siku tano nchini Mexico kueneza nasaha ya kupambana na uhaliofu na rushwa.
Vijana,matumaini ya mustakbal mwema wa Mexico
Leo hii,mnamo siku ya nne ya ziara hiyo,kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni anaelekea katika jimbo la magharibi Michoacan ambako wakulima walisimama kidete mwaka 2013 dhidi ya magengi ya wenye kuuza madawa ya kuleva. Katika mji mkuu wa jimbo hilo Morelia,Papa Francis atakutana na vijana anaowataja kuwa "matumaini ya mustakbal mwema wa nchi hiyo inayogubikwa na mapambano kati ya makundi ya wauza madawa ya kulevya.
Papa Francis amepangiwa kuongoza misa pamoja na wakuu wa kanisa,na watawa na kutilia mkazo msimamo wake kuelekea kanisa. Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni atakamilisha ziara yake kesho jumatano kwa kuutembelea mji wa mpaka wa kaskazini Ciudad Cuarez.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFR
Mhariri.Yusuf Saumu