Papa Francis aanza rasmi ziara yake katika Falme za Kiarabu
4 Februari 2019Mrithi wa mfalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan alimlaki Papa Francis kwenye uwanja wa ndege akiwa na tabasamu huku akiongozana na mawaziri wake. Imam mkuu wa msikiti maarufu wa Al-Azhar wa nchini Misri, Ahmed el Tayeba pia alikuwapo uwanja wa ndege kumlaki Baba Mtakatifu. Leo hii Papa Francis na imam el Tayeb watahutubia kwenye mkutano utakaohudhuriwa na wawakilishi wa dini zote. Hapo kesho Papa Francis ataongoza misa itakayokuwa ya kwanza kuongozwa na baba mtakatifu kwenye rasi ya Uarabuni. Waumini wapatao 135,000 wanatarajiwa kuhudhuria misa hiyo ya hadharani.
Baadae leo mgeni huyo kutoka Vatican atautembelea msikiti mkuu na pia atakutana kwa faragha na wazee wa baraza la Waislamu. Papa Francis pia atahudhuria mdahalo wa kimataifa wa dini zote utakaofanyika katikati ya mji wa Abu Dhabi.
Juu ya ziara ya Papa Francis kwenye rasi ya Uarabuni mkurugenzi mtendaji wa asasi ya kupambana na itikadi kali Maqsoud Kruse amesema jambo mahsusi juu ya ziara hiyo ni kwamba inafungua njia ya hatua muhimu kabisa ya mdahalo kati ya tamaduni mbalimbali na muhimu ni kwamba stahamala inafuatiwa pamoja na hatua thabiti.
Kabla ya kuwasili Uarabuni baba mtakatifu alitoa mwito kwa pande zote zinazohusika na mgogoro wa nchini Yemen wa kutekeleza makubaliano ya kusimamisha vita ili mahitaji ya chakula na dawa yaweze kuwafikia watu wanaokabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu usiokuwa na kifani duniani.
Umoja wa Falme za Kiarabu ni mshirika mkuu wa Saudi Arabia katika vita vya nchini Yemen. Hatua ya baba mtakatifu kutoa wito huo kabla ya kuanza ziara ni kuepusha kuwaumbua wenyeji wake. Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki amesema Mungu anasikia vilio vya watoto wanaotaabika chini ya mazingira ya kivita.
Hata hivyo Papa Francis anafanya ziara kwenye rasi ya Uarabuni wakati ambapo pana mivutano katika ukanda huo. Misiri, Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za nchi za kiarabu zimeisusia Qatar tangu mwaka 2017.
Mwandishi:Zainab Aziz/AP/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga