Papa Benedikt ziarani Ujerumani
22 Septemba 2011Baada ya kupokewa na Rais Christian Wulff na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani atakuwa na mazungumzo pamoja na wanasiasa hao wawili. Mchana atahutubia bunge la Ujerumani - jambo lililozusha mabishano nchini humu. Leo jioni atasoma misa katika uwanja mkubwa wa michezo jijini Berlin na zaidi ya watu 70,000 wanatazamiwa kushiriki katika misa hiyo.
Miji mingine itakayotembelewa na Papa Benedikt ni Erfurt, Thüringer Eichsfeld na Freiburg. Ulinzi wa usalama umeimarishwa katika miji hiyo yote mpaka siku ya Jumapili. Hii ni ziara ya tatu kufanywa na Papa Benedikt nyumbani kwake Ujerumani tangu alipochaguliwa kiongozi wa Kanisa Katoliki katika mwaka 2005 na ni ziara yake ya kiserikali ya kwanza nchini humu.