1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedikt XVI amewasili Uturuki kwa ziara ya siku nne

P.Martin28 Novemba 2006

Baba Mtakatifu Benedikt XVI hii leo anafanya ziara yake ya kwanza katika nchi yenye Waislamu wengi-Uturuki.

https://p.dw.com/p/CHL6

Kabla ya kuondoka uwanja wa ndege mjini Rom,kiongozi mkuu wa Wakatoliki duniani alisema hii ni ziara ya mazungumzo,udugu na usuluhishi.

Lengo la ziara yake ya siku nne nchini Uturuki amesema ni kuboresha uhusiano na Waislamu na pia Wakristo wa Ki-Orthodox.Akasisitiza kuwa hii si ziara ya kisiasa bali ni ya mchungaji na hivyo azma yake ni kuwa na mazungumzo na kushughulikia amani kwa pamoja.

Itakumbukwa kuwa mwezi wa Septemba,matamashi ya Papa yaliwahamakisha Waislamu sehemu mbali mbali za dunia.Katika hotuba aliyoitoa mjini Regensburg wakati wa ziara yake nchini Ujerumani,alimnukulu mfalme wa karne ya kale Byazantine,aliehusisha Uislamu na matumizi ya nguvu.Baadae Papa alisema kuwa amesikitishwa kwamba matamshi yake yamesababisha huzuni lakini hakuomba msamaha kamili.

Licha ya zaidi ya Waislamu 20,000 kuandama mjini Istanbul siku ya Jumapili kuipinga ziara ya Papa nchini Uturuki,Papa Benedikt amesema,anatazamia kupokewa kwa ukunjufu.Akaongezea kusema kuwa Waturuki ni wakarimu,ni watu wanaotaka amani. Daima Uturuki ilikuwa daraja kati ya tamaduni, mahala pa mikutano na mazungumzo.

Hali ya usalama imeimarishwa vikali katika mji wa Ankara,ambao ni kituo cha kwanza cha ziara ya Papa ya siku nne nchini Uturuki.

Kinyume na ilivyotarajiwa hapo awali,sasa imethibitishwa kuwa waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekubali kukutana na Papa kwa muda mfupi kwenye uwanja wa ndege kabla ya kiongozi huyo kuelekea Riga nchini Latvia, kuhudhuria mkutano wa kilele wa shirika la kujihami la magharibi-NATO.

Hatua hiyo imekaribishwa na Vatikan na imesema kuwa ni ishara njema.

Kwa upande mwingine,msemaji wa serikali ya Uturuki,Jumatatu jioni alisema ni matumaini yake kuwa ziara ya Papa itafungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Uislamu na Ukristo.