Papa Benedict wa XVI azikwa huko Vatican
5 Januari 2023Papa mstaafu Benedict XVI amezikwa katika kanisa hilo la Mtakatifu Petro baada ya ibada ya misa iliyongozwa na Kiongozi wa sasa wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis. Benedict ambaye jina lake halisi ni Joseph Ratzinger, sasa amepumzishwa kwenye kaburi la mtangulizi wake aliyekuwa raia wa Poland John Paul II, ambaye mabaki yake tayari yalihamishiwa mahali pengine kanisani hapo miaka kadhaa iliyopita.
Kulingana na Vatican, takriban waumini 50,000 walijiunga na ibada ya mazishi katika uwanja wa Mtakatifu Petro.
Ujumbe mkubwa kutoka Jimbo la Bavaria la Ujerumani, ambako ndiko asili ya Papa Benedict, ulisafiri kwenda Roma kushiriki ibada hiyo ya mazishi. Kansela Olaf Scholz, Rais Frank-Walter Steinmeier, Kiongozi Mkuu wa Bavaria Markus Söder pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri wa Ujerumani walihudhuria pia.
Soma zaidi: Papa Francis aongoza ibada ya mazishi ya Papa Mstaafu Benedict XVI
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ametoa heshima zake za mwisho kwa hayati Papa Benedict XVI na kumtaja kuwa mwanateolojia bora na mwenye unyenyekevu mkubwa.
Benedict alikuwa Papa wa kwanza wa Kanisa Katoliki kujiuzulu katika kipindi cha miaka 600, lakini Steinmeier amesema kujiuzulu kwake hakujaiondoa heshima aliyokuwa nayo duniani kote.
Papa Francis ambaye aliongoza ibada hiyo ya mazishi amesema:
"Tukizingatia kauli ya mwisho ya Bwana na ushuhuda wa maisha yake yote, sisi pia, kama jumuiya ya kanisa, tunahitaji kufuata nyayo zake na kumkabidhi ndugu yetu mikononi mwa Baba. Taa ziiangazie mikono hiyo ya rehema kwa mafuta ya Injili ambayo aliionyesha na kuieneza kwa maisha yake yote.”
Historia ya Papa Benedict
Mapema leo, Vatican imetoa historia rasmi ya maisha ya Papa Benedict katika hati fupi iliyoandikwa kwa lugha ya Kilatini na inayofahamika zaidi kama "rogito", ambayo iliwekwa katika jeneza lake kabla ya kufungwa, pamoja na sarafu na medali zilizotengenezwa wakati wa uongozi wake. Hati hiyo ilizingatia pia urathi wa kiongozi huyo mstaafu wa Kanisa Katoliki duniani.
Mada inayohusiana:
Kifo cha Papa Benedict ni pigo kwa wakatoliki wahafidhina ambao walitamani kuona Kanisa likirejea kwenye misimamo ya hapo awali.
Mwishoni mwa mazishi ya Papa Benedict, kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Papa Paul II, umati wa watu ulipiga kelele kwa Kiitaliano na kusema "Santo Subito!" wakitaka Papa Benedict kutangazwa kama mtakatifu.
Mapapa watatu kati ya watano wa miaka ya hivi karibuni ndio pekee waliotangazwa kuwa watakatifu, lakini kwa jumla karibu theluthi moja ya mapapa wote wametangazwa kuwa watakatifu katika historia ya miaka 2,000 ya Kanisa Katoliki.