1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa awataka Wakristu kutopenda mali na madaraka

25 Julai 2013

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, amewataka Wakristu Wakatoliki kuachana na kile alichokiita kupenda mali na madaraka.

https://p.dw.com/p/19DyC
Papa Francis
Papa FrancisPicha: Reuters

Wito huo ameutoa wakati akiadhimisha Ibada ya Misa katika Pango Takatifu huko Aparecida, kwenye jimbo la Sao Paulo nchini Brazil.

Akihubiri wakati wa Ibada ya Misa yake ya kwanza kuadhimisha tangu awasili Brazil, katika Kanisa Kuu la madhabahu ya Mama Bikira Maria wa Aparecida, Baba Mtakatifu Francis, amewasihi Wakatoliki na hasa vijana wajiepushe kufata njia zinazopotosha na hatimaye kuwaweka njia panda.

Amesema siku hizi watu wamekuwa wakivutiwa zaidi na starehe, mafanikio, utajiri na madaraka na hivyo kuwasihi wazingatie suala zima la imani na ukarimu, ili kurejesha matumaini yanayoanza kupotea miongoni mwa jamii.

Mahujaji vijana wanaohudhuria kongamano lao Brazil
Mahujaji vijana wanaohudhuria kongamano lao BrazilPicha: Getty Images

Amesema amemuomba Mama Maria aliyempenda na kumtunza Yesu awasaidie watu wote wakiwemo viongozi wa Kanisa, wazazi na walimu, ili waweze kufikisha ujumbe wa maadili mema kwa vijana, ambao utawasaidia kulijenga taifa na dunia itakayozingatia haki, usawa, umoja na udugu.

Maelfu wabarikiwa

Baada ya Ibada ya Misa, Baba Mtakatifu alisali tena kwenye Pango la Mama Maria wa Aparecida na kisha akawabariki maelfu ya waumini waliokuwa nje ya Kanisa Kuu na kutangaza kwamba atarejea tena Aparecida mwaka 2017, wakati wa kuadhimisha miaka 300 ya mvuvi aliyeiokota picha nyeusi ya Mama Maria, karibu na mto.

Kisha Papa huyo, alirejea mjini Rio de Janeiro, ambapo alifungua hospitali ya Mtakatifu Francis wa Asizi kwa ajili ya wagonjwa wa akili na hasa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya, iliyopo mjini Rio de Janeiro.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema kuwa tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni janga kubwa katika eneo la Amerika ya Kusini. Amesema jukumu kubwa lililoko sasa ni kuwaelimisha vijana maana na tunu za maisha ya pamoja, pamoja na kuendelea kuwasaidia walioathirika na dawa hizo.

Shughuli za Papa siku ya leo (25.07.2013)

Leo, Baba Mtakatifu ambaye yuko nchini Brazil kwa ziara ya wiki nzima, ataianza siku yake kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye makaazi yake ya muda huko Sumare, Rio de Janeiro na kisha atapewa ufunguo wa mji huo pamoja na kubariki bendera za Olimpiki.

Papa Francis akiongoza Misa, Aparecida, Brazil
Papa Francis akiongoza Misa, Aparecida, BrazilPicha: Reuters

Aidha, Papa atatembelea eneo la mitaa ya mabanda na baadae jioni atawakaribisha zaidi ya vijana milioni moja kutoka sehemu mbalimbali duniani katika ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Kikatoliki Duniani kwa mwaka wa 2013. Shughuli hiyo itafanyika katika ufukwe wa Copacabana, huko Rio de Janeiro.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu ametoa pole kwa familia za watu waliopoteza maisha katika ajali ya treni iliyotokea nchini Uhispania jana. Abiria wengi katika treni hiyo, walikuwa mahujaji wanaoelekea Santiago de Compostela, kuhudhuria sherehe za mtakatifu msimamizi wa mji huo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,DPAE
Mhariri: Josephat Charo