Papa aukosoa vikali uongozi wa Vatican
23 Desemba 2014Katika orodha ya madhambi saba makubwa zaidi ya Kanisa Katoliki, Papa Francis ameongeza kile alichokiita magongwa 15 yanayowakabili wasaidizi wake ndani ya Vatican, na kuwataka watumie muda huu wa Krismas kutubu dhambi zao na kulifanya Kanisa kuwa mahala penye afya na patakatifu zaidi mwaka 2015.
Papa Francis alizungumza juu ya wale wanaojigeuza kuwa mabosi, na wanaojiona wako juu ya kila mmoja na hawamtumikii yeyote. Alionya pia juu ya kile alichokiita "ugonjwa wa madaraka" na kuwaonya dhidi ya nargisi ya wale wanaojijali wenyewe bila kuwahurumia walio dhaifu na wanaohitaji zaidi.
Tamaa ya vyeo na ubinafsi
Aliwakosoa pia wasiowaheshimu wakubwa zao akisema,"ugonjwa wa kutomtii mkubwa ndiyo ugonjwa wa wale wanaowasifu wakubwa zao wakitumai kupata kitu kutoka kwao. Hao ni wahanga wa tamaa ya vyeo na ubinafsi, wanawaheshimu binaadamu na siyo Mungu."
Na wakati miongoni mwa wasikilizaji walikuwepo waliokunja sura zao, papa alizungumzia ugonjwa wa kile alichokiita sura za msiba, akibainisha kuwa watu wasioridhika na wanaokunja sura, wale wanaojaribu kuva sura za ukali, wanawatendea wengine, hasa wale wanaoamini ni wa hadhi ya chini, kwa dharau na kwa kibri.
Francis ambaye ndiye papa wa kwanza kutoka Amerika Kusini na hakuwahi kufanyakazi katika baraza la uongozi wa kanisa hilo linalodhibitiwa na Wataliana kabla ya kuchaguliwa, hakuona haya kulalamika juu ya porojo, tamaa ya vyeo, na hila za madaka vinavyoikabili Vatican. Lakini wakati ajenda yake ya mageuzi ikizidi kushika kasi, alionekana mwenye kuthubutu zaidi hata kuweza kubainisha yale yanayoikwamisha taasisi hiyo.
Hotuba kali zaidi
Wafuatiliaji wa masuala ya Vatican walisema hawajawaji kusikia hotuba kali kama hiyo kutoka kwa papa, na kuongeza kuwa huenda ameamua kuweka mambo hadharani kutoka na upinzani anaokabiliana nao katika kutekeleza mageuzi yake.
"Ukweli kwamba anaielekeza hotuba yake ya Krismas kwa magonjwa 15 ya kiroho kwa namna hiyo, kwa maoni yangu ni ishara kwamba anachukulia mageuzi katika uongozi, na mageuzi ya kiroho kiujumla, kama hatua muhimu anayotaka kuendelea kuchukuwa, kwamba bado kuna upinzani mkubwa,na kwamba pengine upinzani umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni," alisema Iacopo Scaramuzzi, ripota wa gazeti la TMNews mjini Vatican.
Mwanahistoria wa kanisa katika chuo kikuu cha Seton Hall Padri Robert Wister, alisema kimsingi Papa Francis alikuwa anaomba wasaidizi wake wajitathmini wenyewe, akiwaomba kuangalia namna walivyotenda dhambi mbele ya Mungu kabla ya kwenda kutubu. Aliongeza kuwa pengine anaamini karipio kali linaweza kusaidia kubadili mambo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,dpae
Mhariri: Charo Josephat