Papa atoa wito wa dunia bila silaha za kinyuklia
24 Novemba 2019"Eneo hili linatufanya kutambua maumivu na maovu ambayo sisi binadamu tunaweza kufanyiana," Francis alisema katika eneo la uwanja wa kumbukumbu ya mabomu ya atomiki mjini Nagasaki huku mvua ikinyesha.
Kabla ya hotuba yake, papa alitoa heshima zake kwa wahanga wa shambulio la Marekani la bomu la nyuklia mwaka 1945 katika mji huo wa kusini magharibi nchini Japan, na kuwauwa watu 74,000, ikiwa ni pamoja na maelfu ya wakatoliki.
"Hapa katika mji huu ambao ulishuhudia madhila ya maafa ya kibinadamu na mazingira kutokana na shambulio la nyuklia, juhudi zetu kuzungumzia dhidi ya mashindano ya silaha hazitatosha," amesema Francis, ambaye ameanza ziara yake ya siku nne nchini Japan siku ya Jumamosi.
Shambulio la mji wa Nagasaki Agosti 9, 1945, lilikuja siku tatu baada ya shambulio la kwanza la bomu la atomiki lililodondoshwa na ndege ya mashambulizi ya B-29 ya Marekani na kuripuliwa katika mji wa Hiroshima, na kusababisha watu 140,000 kuuwawa.
Amani na uthabiti
"Moja kati ya kile moyo wa binadamu inachopenda zaidi ni usalama, amani na uthabiti. Kuwa na silaha za nyuklia na silaha nyingine za maangamizi sio jibu la hisia hizi moyo wa binadamu unavyopenda, kwa kweli kila mara binadamu anajaribu kuzuwia hilo," amesema papa mwenye umri wa miaka 82.
"Amani na uthabiti wa kimataifa hayalingana na majaribio ya kujenga juu ya hofu ya uharibifu wa pamoja ama kitisho cha maangamizi ya jumla," amesema.
Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutia saini na kuidhinisha mkataba wa kuzuwia silaha za kinyuklia, ambao uliidhinishwa na mataifa 122 mwezi Julai 2017.
Hata hivyo, mkataba huo bado haujaanza kutumika kwa kuwa haujaidhinishwa na mataifa 50 ambayo yanatakiwa kutia saini.
Wanaharakati wa kupinga silaha za kinyuklia wameitaka Japan, nchi pekee ambayo imeathirika na mashambulizi ya silaha za atomiki, kutia saini na kuidhinisha mkataba huo haraka iwezekanavyo.
Lakini serikali ya waziri mkuu Shinzo Abe hadi sasa imekataa kufanya hivyo wakati nchi hiyo ikiwa chini ya mwamvuli wa kinyuklia wa Marekani.
Dunia bila silaha za kinyuklia
"Nikiwa naamini kuwa dunia bila silaha za kinyuklia inawezekana na ni muhimu, nawataka viongozi wa kisiasa kutosahau kuwa silaha hizi haziwezi kutulinda kutokana na kitisho cha hivi sasa katika usalama wa kitaifa na kimataifa," amesema Papa.
"Tunahitaji kutafakari athari za maafa ya uwepo wake,hususan kutokana na mtazamo wa kiutu na mazingira, na kukataa kuongeza hofu ya kimazingira, kutokuaminiana na uhasama unaochochewa na nadharia za nyuklia".
Papa atafanya ibada ya misa katika uwanja wa michezo mjini Nagasaki baadaye mchana na kisha atasafiri kwenda Hiroshima, ambako "mkutano kwa ajili ya amani" umepangwa kufanyika.
Siku ya Jumatatu , Francis anatarajiwa kufanya mkutano na mfalme Naruhito, ambaye ameingia madarakani Mei mosi, na waziri mkuu mjini Tokyo.
Papa pia atakutana na wahanga wa tetemeko la ardhi la mwaka 2011, tsunami na maafa ya nyuklia kaskazini mashariki mwa Japan.
Ziara yake inakuwa ya kwanza kufanywa na papa nchini Japan katika muda wa miaka 38. Mwaka 1981 papa John Paul 11 alikwenda Hiroshima, Nagasaki na Tokyo.