1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Panetta akwaruzana na Karzai kuhusu vita vya Afghanistan

6 Oktoba 2012

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panetta amemtaka rais wa Afghanistan Hamid Karzai kuvishukuru vikosi vya Umoja wa Kujihami, NATO vinavyopigana na kufia nchini humo badala ya kuvikosoa.

https://p.dw.com/p/16LUS
Rais Hamid Karzai akiwa na waziri Leon Panetta mjini Kabul.
Rais Hamid Karzai akiwa na waziri Leon Panetta mjini Kabul.Picha: Reuters

Panetta aliyekuwa katika ndege ya jeshi la Marekani alisema mafanikio yaliyopo nchini Afghanistan kwa sasa yamegharimu maelfu ya maisha ya wanajeshi wa kimataifa, na kwamba itakuwa ni busara kwa rais Karzai kutoa shukrani kwa kujitolea huko. "Tumepata mafanikio nchini Afghanistan kwa sababu kuna wanaume na wanawake waliyovalia sare ambao walikuwa tayari kupigana na kufa kwa ajili ya uhuru wa Afghanistan, na haki yao ya kujitawala na kuwa salama," alisema Panetta wakati wa safari yake kuelekea nchini Peru.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta akizungumza katika mkutano na rais hamid Karzai mjini Kabul hivi karibuni.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta akizungumza katika mkutano na rais hamid Karzai mjini Kabul hivi karibuni.Picha: dapd

Panetta alibainisha kuwa wanajeshi 2,000 wa Marekani walikuwa miongoni mwa waliyouawa katika vita vilivyoongozwa na Marekani, washirika wa NATO na serikali ya Afghanistan, na kuongeza kuwa maafisa hao wamekufa wakati wakipambana na adui sahihi. "Na nadhani itakuwa busara kama rais mara moja moja ataonyesha shukurani kwa kujitoleam kwa wanajeshi hao walliyopigana na kuuawa Afghanistan, kuliko kuwakosoa tu," alisema Panetta.

Karzai asema Marekani ni ndumila kuwili

Matamshi hayo yamekuja siku moja baada ya rais Hamid Karzai kuuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Kabul kuwa Marekani ilikuwa inacheza mchezo wa ndumila kuwili nchini mwake kwa kupigana vita katika vijiji vya Afghanistan badala ya kuwfuata wanaowaunga mkono wanamgambo ambao alidai wako nchini Pakistan."NATO na Afghanistan wanapaswa kupigana vita hivi kule ambako ndiyo chimbuko la ugaidi," alisema Karzai katika matamshi yaliyochapishwa na gazeti la New York Times na kuongeza kuwa, "Lakini Marekani haiko tayari kwenda kupambana na magaidi huko. Hii inaonyesha undumila kuwili. Wanasema kitu kimoja na wanafanya kingine."

Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka baina ya Marekani na Afghanistan katika siku za hivi karibuni, ikichochea kwa upande moja na ongezeko la mashambulizi ya wanajeshi wa Afghanistan dhidi ya vikosi vya Marekani na washirika wake wa kimataifa, na pia wasiwasi juu hatma ya nchi hiyo baada ya kuondolewa kwa vikosi hivyo vya kimataifa mwishoni mwa mwaka 2014. Matamshi ya Panetta aliyatoa wakati wa safari itakayompeleka nchini Peru kwa mazungumzo ya usalama baina ya mataifa hayo mawili, na baadaye nchini Uruguay kuhudhuria mkuitano wa mawaziri wa ulinzi kutoka Amerika. Baadaye Panetta atasafiri kwenda mjini Brussels, Ubelgji kuhudhuria mkutano wa NATO kuhusu Afghanistan na mambo mengine.

Karzai na Panetta wakiwa katika mazungumzomengine mjini Kabul.
Karzai na Panetta wakiwa katika mazungumzomengine mjini Kabul.Picha: Reuters

Kuuhakikishia mkutano wa NATO

Panetta alisema ataihakikishia NATO kuwa Jenerali John Allen, kiongozi wa vikosi vya kimataifa nchini Afghanistan alikwa akishirikiana na waafghanistan kushughulikia tatizo la mashambulizi ya ndani na kwamba ni muhimu kuendelea na mpango wa Allen wa kuanza kupunguza vikosi ifikapo mwaka 2014. Waziri huyo wa Ulinziwa Marekani alisema kuporomoka hivi karibuni, kwa thamani ya sarafu ya Iran na vurugu zinazoendela nchini humo, ni ishara kuwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Iran juu ya mpango wake wa nyuklia vilikuwa vinafanya kazi.

Alipoukizwa kuhusu hasira za waasi wa Syria juu ya kushindwa kwa nchi za magharibi kuingilia kati mgogoro huo kusaidia kuungusha utawala wa rais Bashar al-Assad, Panetta alisema mgogoro huo ni mgumu na wenye kutoa changamoto. Alisema Marekani ilikuwa inatoa msaada usio wa kijeshi na kushirikiana na nchi nyingine katika kanda ya mashariki ya kati yanayowapatia waasi hao msaada usiyo wa kijeshi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Sekione Kitojo