Pande zinazozozana Sudan zakubali kusitisha vita kwa saa 24
9 Juni 2023Hayo yamesemwa na wapatanishi wa Marekani na Saudi Arabia ambao wamesema majaribio ya awali ya kusitisha mzozo huo unaokaribia sasa mwezi wa tatu yamekuwa yakivunjika.
Kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia, wawakilishi wa pande zinazozozana nchini Sudan, likiwemo jeshi la taifa SAF na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), wamekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa saa 24 kote nchini humo kuanzia kesho Jumamosi saa kumi na mbili asubuhi.
Pande hasimu Sudan kurejea kwenye meza ya mazungumzo
Makubaliano kadhaa ya kusitisha vita hapo nyuma yamekuwa yakivunjika. Mnamo mwisho wa mwezi Mei, Marekani iliwawekea vikwazo majenerali wanaohasimiana wa pande hizo mbili, ikiwashutumu kwa kile ilichokiita umwagaji damu wa kutisha.
Wapatanishi wamesema endapo pande zinazozozana hazitaheshimu makubaliano ya sasa hivi, basi huenda wajumbe wa juhudi za upatanishi watatafakari kusitisha tena mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Jeddah Saudi Arabia.
Tangu Aprili, mapigano kati ya jeshi na kikosi cha RSF, yamekuwa yakiendelea mara kwa mara katika mji mkuu Khartoum na jimbo la magharibi Darfur huku pande husika zikikiuka makubaliano ya usitishaji vita yanayolenga pia kutatua tatizo la mgogoro wa kibinadamu.
Machafuko ya Sudan yamewaua watu 1,800
Kulingana na shirika linalofuatilia mizozo inayohusisha silaha (ACLED), zaidi ya watu 1,800 wameuawa. Umoja wa Mataifa nao umesema takriban watu milioni mbili wamekimbia makaazi yao, wakiwemo 476,000 ambao wamekimbilia nchi jirani kama wahamiaji.
Wapatanishi wa Marekani na Saudi Arabia wamesema wanafadhaishwa vilevile saw ana raia wa Sudan kuhusu kutotekelezwa kwa makubaliano yaliyopita ya usitishaji vita.
Mapigano yaendelea kushuhudiwa nchini Sudan
Taarifa hiyo ya Saudi Arabia imesema, ikiwa makubaliano hayo yataheshimiwa, basi itatoa nafasi muhimu kwa pande husika kuchukua hatua za kujenga Imani, ambayo itaruhusu kurejeshwa kwa mazungumzo ya Jeddah.
Sudan yasema mjumbe wa UN Volker Perthes hakaribishwi nchini humo
Tangazo la Ijumaa limejiri siku moja tu baada ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini Saudi Arabia, ambako alifanya mazungumzo na maafisa wakuu wa taifa hilo kuhusu Sudan.
Taarifa hiyo imejiri siku moja pia baada ya utawala wa kijeshi wa Sudan kutangaza kuwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes, hakaribishwi tena nchini mwao, wakimshutumu kwa kuegemea upande mmoja.
Mapigano hayo yameweka kando juhudi za mjumbe huyo za kufufua mchakato wa mpito wa Sudan kurejesha utawala wa kiraia ambao ulikatizwa na mapinduzi ya 2021 ya majenerali hao wawili kabla ya kutofautiana.
Chanzo: AFPE