1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande mbili hasimu Lebanon zakusanyika mji mkuu.

Abdulrahman, Mohamed14 Februari 2008

Wanajeshi nchini Lebanon waweka ulinzi mkali mjini Beirut.

https://p.dw.com/p/D7Mx
Waziri mkuu wa zamani aliyeuawa rafik HaririPicha: AP

Mikusanyiko hiyo mjini Beirut ni ule wa wafuasi wa serikali upande mmoja na upinzani upande wa pili.

Wakati Washia wanaokiunga mkono chama cha Hezbollah wanamuaga kamanda wa ngazi ya juu wa kundi hilo Imad Mughniyeh aliyeuwawa jana katika mji muu wa Syria-Damascus ,wapinzani wao na wafuasi wa serikali wanakusanyika kumkumbuka Waziri mkuu wa zamani Rafik Hariri aliyeuwawa mwaka 2005.


Kukiwa na hofu ya uwezekano wa kuzuka machafuko baina ya wafuasi wa pande hizo mbili zinazohasimiana, maafisa nchini Lebanon wameweka maelfu ya wanajeshi na vizuzi katika barabara kuu za mji wa Beirut. Chama cha msimamo mkali cha Hezbollah kimewataka wafuasi wake kumiminika katika ngome yake kuu kusini mwa Beirut na kuandamana nyuma ya jeneza la Imad Mughniyeh, aliyekua mkuu wa usalama wa kundi hilo na mmoja kati ya wanaharakati waliokua wakisakwa kwa muda mrefu duniani. Mughniyeh aliuwawa katika mripuko wa bomu lililotegawa garini jana, katika mji mkuu wa Syria Damascus.


Viongozi wa Hezbollah, kundi linaloungwa mkono na Syria na Iran wameitwika dhamana Israel kwa mauaji hayo, lakini maafisa wa Israel wamekanusha kuhusika kokote na tukio hilo, ingawa wamesema wamefurahishwa na kifo cha kamanda huyo, maoni ambayo yanafanana na msimamo wa Marekani kuhusiana na tukio hilo ,ikisisitizwa kwamba ni ushindi katika vita dhidi ya ugaidi.


Mughniyeh amehusishwa na mashambulio kadhaa dhidi ya nchi za magharibi na Israel katika miaka ya 1980 na 90.

Alikua akisakwa pia kuhusika na hujuma ya bomu kwenye ubalozi wa Israel mjini Buenos Aires Argentina 1992 ambapo watu 29 waliuwawa na ile ya 1994 katika kituo cha jamii ya Wayahudi, shambulio lililowauwa watu 85 na wengine 30 kujeruhiwa.


Kwa upande mwengine. wakati wafuasi wa Hezbollah wakikusanyika katika maziko ya Mughniyeh, wapinzani wao nao wamekusanyika kumkumbuka waziri mkuu wa zamani Rafik Hariri aliyeuawa 2005 katika shambulio la bomu liliklotegwa garini. Syria inashutumiwa kuhusika na mauaji hayo , lakini imekanusha madai hayo.

mwanamke mmoja alisikika wakipiga kelele"tunataka uchaguzi wa rais na tunataka mahakama ya kimataifa."

Uchunguzi wa wataalamu wa umoja wa mataifa, umewahusisha watu kadhaa katika kifo cha waziri mkuu huyo wa zamahni lakini bado hakuna aliyeshtakiwa.


Matukio yote haya hii leo yanakuja katika wakati ambapo Lebanon bado imo kwenye mgogoro wa kisiasa, unaotokana na kushindwa kwa pande zinazohasimiana kubaliana juu ya rais mpya tokea ulipomalizika muda wa rais Emile Lahoud kumalizika mwezi Novemba na kutangaza analikabidhi jeshi usalama wa taifa hilo.

Tangu wakati huo serikali inayoongozwa na Waziri mkuu msunni Fouad Siniora anayeungwa mkono na nchi za magharibi na upinzani unaoongozwa na chama cha washia- Hezbollah zimeshindwa kuafikiana juu ya rais mpya ambaye kikatiba lazima atoke katika jamii ya wakristo wa madhehebu ya mironite na vikao kadhaa vya bunge vilivyoitishwa kujaribu kumchagua rais mpya vimeahirishwa.