Pande hasimu Libya zashindwa kuafikiana juu ya uchaguzi
20 Juni 2022Pande mbili zinazohasimiana nchini Libya zimeshindwa kufikia makubaliano baada ya kumaliza duru ya tatu ya mazungumzo ya upatanishi yaliyoongozwa na Umoja wa Mataifa nchini Misri kuhusu uchaguzi, na kuzidisha mkwamo wa kutafuta suluhu ya machafuko ya muongo mmoja nchini humo. Kwa mujibu wa mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Stephanie Williams, wabunge kutoka eneo la mashariki linaloongozwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar na serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa iliyoko mji mkuu wa Tripoli, walihitimisha jana Jumapili duru yao ya mwisho ya mazungumzo kuhusu marekebisho ya katiba juu ya uchaguzi bila ya mafanikio. Mazungumzo hayo, yalioanza Juni 12, yalinuia kuanzisha mfumo wa sheria kwa ajili ya kufanyika uchaguzi lakini pande hizo mbili zimeshindwa kukubaliana juu ya sheria zinazosimamia kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi. Mshauri huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya ametoa wito kwa spika wa bunge mwenye ushawishi mkubwa Aguila Saleh na mkuu wa baraza kwenye serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa Khaled al-Meshri kukutana tena katika kipindi cha siku 10 ili kujaribu kuziba mapengo kati ya pande hizo, japo hakufafanua zaidi.