Palestina yakaribisha mamataifa uchunguzi kifo cha Shireen
15 Mei 2022Kupitia ukurasa wake wa Twitter, afisa mmoja mwandamizi wa Mamlaka ya Palestina, Hussein al-Sheikh, ameandika kwamba mamlaka itaukaribisha ushiriki wa mashirika ya kimataifa katika uchunguzi wake, ingawa imekataa ushiriki wa Israel ambayo inaamini inahusika moja kwa moja na kifo cha mwandishi wa habari, Shireen Abu Akleh.
Polisi ya Israel iliuvamia na kuushambulia msafara wa waombolezaji wa Kipalestina, kwenye eneo la Mji Mkongwe waliokuwa wamebeba jeneza la mwanahabari huyo, tukio ambalo limesababisha jumuiya ya kimataifa kulilaani.
Vurugu hizo ziliongeza hasira kwa Wapalestina baada ya mauwaji ya Shereen, ambayo yametishia kuchochea mivutano ambayo imekuwa ikiongezeka tangu Machi.
Israel yaunda timu ya uchunguzi
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel, Omer Barlev, alisema kuwa yeye na kamishna wa polisi wamekwishateua jopo la kufanya uchunguzi wa kina wa kile kilichotokea wakati wa mazishi na kwamba matokeo ya uchunguzi huo yatatolewa katika siku zijazo.
Mamlaka ya Palestina imekielezea kifo cha mwandishi huyo wa habari, ambaye alikuwa akiripoti uvamizi wa Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu, kama tukio la mauaji la vikosi vya Israel.
Awali Israel ilitaka kuonesha kuwa huenda mashambulizi ya Palestina ndio chanzo cha kifo, lakini pia maafisa wamesikika wakisema hawawezi kuuondoa uwezekano wa mwanahabari huyo kuuwawa kwa mashambulizi ya Israel.
Katika ripoti yake, Baraza la Usalama la Umoja wa Ulaya limeyalaani vikali mauwaji hayo na kutoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka, wenye uwazi, wa haki na usioegemea upande wowote.
Vurugu katika mazishi ya Shireen
Katika tukio la siku ya Ijumaa (Mei 13), polisi ya Israel iilidai kuwa ilikuwa ikifanya jitihada za kufanikisha mazishi yenye amani na staha na kwamba ilishiriki katika uratibu wake na familia ya marehemu, "lakini kwa bahati mbaya, mamia ya waouvu walifanya jaribio la kuvuruga utaratibu wa shughuli hiyo na kuwadhuru polisi.
Soma zaidi:Ripota wa Aljazeera auawa katika uvamizi wa Israel Ukingo wa Magharibi
Katika taarifa nyengine, Mpalestina mmoja alifariki dunia siku ya Jumamosi (Mei 14) kufuatia majeraha yaliyotokana na makabiliano na vikosi vya usalama vya Israel wiki tatu zilizopita katika viwanja vya msikiti wa al-Aqsa.
Kifo hicho kimeingia katika rikodi ya kuwa cha mwanzo kutokea katika eneo takatifu kwa miaka kadhaa.
Chanzo: RTR