1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PALERMO: Michezo yote ya mpira imepigwa marufuku Italia

3 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCVV

Jumuiya ya Kandanda nchini Italia imefuta michezo yote ya mpira ya ligi na kimataifa,kwa muda usiojulikana.Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kutokea kifo cha afisa mmoja wa polisi katika ghasia zilizozuka mwishoni mwa mchezo,kati ya vilabu vya Catania na Palermo.Afisa huyo aliekuwa ndani ya gari ya polisi,alirushiwa bomu la kienyeji.Watu 100 vile vile wamejeruhiwa katika machafuko hayo.Kifo hicho ni cha pili kutokea nchini Italia kuhusika na soka,katika kipindi cha juma moja.Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Kandanda ya Italia imesema,michezo haitoruhusiwa mpaka yatakapopatikana makubaliano ya kuchukuliwa hatua mpya zilizo imara,ili kuzuia matokeo ya aina hiyo katika siku zijazo.Mkutano wa dharura umepangwa kufanywa siku ya Jumatatu.Mawaziri wa ndani na spoti vile vile wanatazamiwa kuhudhuria mkutano huo.Waziri mkuu wa Italia Romano Prodi vile vile ameunga mkono uamuzi uliopitishwa na Jumuiya ya Kandanda nchini humo.