1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yarusha makombora ya kulipiza kisasi Iran

18 Januari 2024

Pakistan imesema imetumia droni zinazoweza kusababisha mauaji na maroketi kuwashambulia wanamgambo wa Balochistan ndani ya Iran.

https://p.dw.com/p/4bQsh
Pakistan, Islamabad | Mumtaz Zahra Baloch
Msemaji wa wizara ya kigeni wa Pakistan Mumtaz Zahra Baloch Picha: Muhammet Nazim Tasci/Anadolu/picture alliance

Hili ni shambulizi la kulipiza kisasi siku mbili baada ya Iran kusema kwamba imeshambulia kambi mbili za kundi jengine ndani ya mpaka wa Pakistan.

Vyombo vya habari nchini Iran vinasema makombora kadhaa yamekishambulia kijiji kimoja katika mkoa wa Sistan-Baluchestan unaopakana na Pakistan, na kusababisha vifo vya karibu watu 9 wakiwemo watoto 4.

Mzozo mpya waibuka kati ya Pakistan na Iran

Majirani hao wamekuwa na mahusiano ya kusuasua katika miaka iliyopita ila mashambulizi hayo ya mpakani ndiyo makubwa zaidi kuwahi kufanyika baina ya nchi hizo katika miaka ya hivi karibuni na yanafanyika huku kukiwa na wahaka unaozidi kuongezeka kuhusiana na hali ya usalama ya eneo la Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas mnamo Oktoba 7.