1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yajiweka mbali na mzozo wa Iran na Marekani

6 Januari 2020

Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Shah Mehmood Qareshi amesema hii leo kwamba taifa hilo halitajihusisha kwa namna yoyote katika mzozo unaoendelea kufukuta baina ya Marekani na Iran.

https://p.dw.com/p/3VmnZ
Iran Trauerzeremonie für getöteten General Soleimani in Teheran
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Noroozi

Waziri huyo ameliambia bunge la Pakistan kwamba taifa hilo halitajihusisha na juhudi zozote za kuanzisha vita ama kuruhusu ardhi yao kutumika dhidi ya taifa lolote kama sehemu ya sera yao ya kuzuia machafuko kwenye ukanda huo. Mwaka jana waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan alikuwa msuluhishi wa mzozo kati ya Saudi Arabia na Iran.

Pakistan ina eneo la ukubwa wa maili 620 za mpaka wanazogawana na Iran na kwa muda mrefu imejaribu kusawazisha mahusiano na Tehran wakati ikiwakilisha maslahi ya kidiplomasia ya Iran nchini Marekani.  

Wasiwasi unazidi kuongezeka kote Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi hayo ya Marekani dhidi ya Jenerali Qassem Soleimanimjini Baghdad na kuifanya Iran kuapa kulipiza kisasi kikali dhidi ya hasimui wake huyo wa muda mrefu.

Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa kipalestina la Hamas Ismail Haniyeh aliyehudhuria mazishi ya Soleimani mjini Tehran amewahutubia waombolezaji akimtaja kamanda huyo kama shahidi wa kikosi maalumu cha al-Qurds kwenye jeshi la kimapinduzi la Iran.

Amesema, "Ninatangaza kwamba, upinzani uliosababisha ushindi huko Lebanon na Gaza, kwa hakika utasababisha ushindi kwenye vita vigumu dhidi ya uzayuni. kwa uwezo wa Mungu aliye mkuu." 

China Wuhan 2019 | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atazungumza na rais Vladimir Putin wa Urusi kujadili masuala ya Mashariki ya KatiPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Katika hatua nyingine, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Jumamosi hii atakwenda Urusi kukutana na rais Vladimir Putin. Kulingana na msemaji wa kansela, Steffen Seibert, Merkel na Putin watajadili masuala ya kimataifa yanayojitokeza wakati huu ambayo ni pamoja na Syria, Libya, Iran, Iraq, Ukraine pamoja na mahusiano baina ya mataifa hayo.

Merkel amekwishazungumza na rais wa Uturuki, Recep Tayyipp Erdogan hii leo kuhusu hali ya mambo kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati. Ujerumani imesema iko tayari kusuluhisha mzozo kati ya Marekani na Iran kufuatia mauaji ya kamanda Soleimani. Hata hivyo itatakiwa kufanya jitihada za kujihakikisha kwamba inakuwa msuluhishi mwaminifu kwenye mzozo huo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwenye kikao cha baraza la mawaziri hii leo amekosoa kile alichotaja "nia ovu za Iran" pamoja na uamuzi wake wa kuachana na mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa serikali Sibeth Ndiaye.

Macron ametoa mwito wa kuondolewa kwa hali ya wasiwasi kufuatia matukio ya hivi karibuni. Ufaransa ina wanajeshi 1,000 wanaopambana na IS nchini Iraq na Syria.

Huko Iraq viongozi waandamizi wamekusanyika mjini Baghdad kupokea salamu za rambirambi kufuatia vifo vya wanajeshi wake waliouawa pamoja na Soleimani. Rais Barham Salih na waziri mkuu wa serikali ya mpito Adel Abdul-Mahdi pamoja na mabalozi wamekusanyika kwenye shughuli hiyo.  

Baraza la wawakilishi la Marekani hapo jana limesema litaanzisha na kupigia kura azimio la kuwekea ukomo hatua za kijeshi za rais Donald Trump dhidi ya Iran.