Pakistan yahitaji msaada wa dharura: UNICEF
3 Agosti 2010Wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto-UNICEF, likitangaza idadi ya watu waliokufa kutokana na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini Pakistan kuwa imefikia zaidi ya 1,400 na wengine kiasi milioni 3.2, wakiachwa bila makaazi, wabunge wa Uingereza wenye asili ya Pakistan wameikosoa ziara ya Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan atakayoianza nchini humo baadae leo.
Kwa mujibu wa shirika hilo la UNICEF, misaada inakawia kuwafikia maelfu ya watu walioko katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa za masika, huku hatari ya kuripuka magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na maji machafu ikizidi kuongezeka. Shirika hilo limefafanua kuwa zaidi ya watu milioni moja wanahitaji msaada wa dharura kutokana na mafuriko hayo mabaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 80 iliyopita. Wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wanahofia kuwa taarifa za kunyesha mvua zaidi zitaifanya hali kuwa mbaya zaidi, kwani hadi sasa helikopta ndio njia pekee ya kuwafikia waathirika ambao wako katika maeneo yaliyozingirwa na mafuriko hayo.
Katika taarifa yake, Kamishna wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi-UNHCR, Antonio Gutteres amesema kuwa hali ya maisha ya watu walioathiriwa na mafuriko hayo iko katika hatari na wanahitaji msaada wa haraka. Msemaji wa UNICEF, Marco Jimenez amewaambia waandishi habari kuwa mafuriko hayo yanasambaa zaidi kuelekea eneo la kusini katika majimbo ya Punjab na Sindh. Jimenez amesema katika watu milioni 3.2 walioathiriwa na mafuriko hayo, watoto ni milioni 1.4. Kwa upande wake Shirika la Mpango wa Chakula duniani-WFP, limesema kuwa kuanzia jana limeanza kugawa chakula kwa ajili ya watu 42,000, huku kiasi watu 250,000 wakitarajiwa kupokea msaada wa chakula cha dharura ifikapo mwishoni mwa wiki hii.
Wakati hayo yakijiri, wabunge wa Uingereza wenye asili ya Pakistan wamemtaka Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan kukatisha ziara yake nchini Uingereza na kurudi nyumbani kwa ajili ya kulishughulikia janga hilo la mafuriko na kuwaunga mkono wananchi wake. Baadhi ya wanasiasa hao hawatahudhuria katika mkutano uliopangwa wa kukutana na Rais Zardari, wakisisitiza kiongozi huyo avunje ziara yake itakayohusu zaidi masuala ya kisiasa na kurejea nyumbani. Zardari baadaye hii leo ataanza ziara ya siku tano nchini Uingereza ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na Waziri Mkuu David Cameron. Kiongozi huyo pia anatarajiwa kukutana na wabunge wa nchi hiyo wenye asili ya Pakistan siku ya Alhamisi na siku ya Jumamosi atahudhuria sherehe ambayo taarifa zinaeleza kuwa ni kwa ajili ya kuzindua mkakati wa kujihusisha kwa mtoto wake wa kiume, Bilawal Bhutto Zardari katika masuala ya kisiasa.
Wabunge hao wamesema fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na kiongozi huyo katika hoteli yenye hadhi kubwa ya kimataifa, zipelekwe Pakistan kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko hayo. Hata hivyo siyo wabunge wote wa Uingereza wenye asili ya Pakistan wamesusia mkutano huo wa mchana. Qassim Afzal kutoka chama cha Liberal-Democrats na Sayeeda Warsi, mwanamke wa kwanza Muislamu kuwepo katika baraza la mawaziri watahudhuria chakula hicho cha mchana. Ziara ya Rais Zardari ilianzia nchini Ufaransa hapo jana ambako alikutana na Rais Nicolas Sarkozy na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Bernard Kouchner.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri:Abdul-Rahman