1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yaamua kutojiunga na kampeini ya kijeshi Yemen

Admin.WagnerD10 Aprili 2015

Bunge la Pakistan limeitaka serikali ya nchi hiyo kujiepusha na mzozo wa Yemen kwa kukataa ombi la Saudi Arabia la kujiunga na kampeini ya kijeshi inayofanywa nchini Yemen dhidi ya waasi wa kishia wa Houthi.

https://p.dw.com/p/1F5n1
Picha: picture-alliance/dpa

Wabunge wa Pakistan wamepiga kura kwa kauli moja ya kuunga mkono ahadi ya serikali ya kuilinda mipaka ya Saudi Arabia ambayo mpaka sasa haiajatishiwa na mzozo unaoendelea Yemen na badala yake bunge hilo la Pakistan limeitaka serikali kujihusisha na juhudi za kidiplomasia kwa kuwa mpatanishi na kutoegemea upande wowote kwa kutojihusisha katika vita vya Yemen.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya bunge la Pakistan kuujadili mzozo wa Yemen kwa siku tano. Hayo yanakuja huku muungano wa kijeshi wa nchi za ghuba zinazoongozwa na Saudi Arabia zikifanya mashambulizi makali zaidi ya angani usiku wa kuamkia leo kusini mwa Yemen tangu kampeini hiyo kuanza wiki mbili zilizopita.

Mashambulizi makali yaripotiwa Aden

Walioshuhudia wamesema operesheni hiyo imeyalenga makao makuu ya serikali ya mitaa katika mtaa wa Dar Saad mjini Yemen, uwanja wa michezo ulioko katikati mwa mji huo na vituo vya ukaguzi vinavyosimamiwa na waasi wa Houthi. Mashambulizi pia yameripotiwa katika mji wa Ataq katika jimbo la Shabwa mashariki mwa Yemen ambao ulidhibitiwa hapo jana na wanajeshi watiifu kwa rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Raia wa Yemen wakitaabika kutfauta maji
Raia wa Yemen wakitaabika kutfauta majiPicha: picture alliance/abaca

Huku hayo yakijiri, ndege mbili zilizobeba misaada ya vifaa vya matibabu za mashirika ya msalaba mwekundu na shirika la kushughulikia maslahi ya watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF zimetua katika mji mkuu wa Yemen Sanaa, hii leo zikiwa na tani 30 ya vifaa hivyo vya matibabu.

Mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada yamekuwa yakijaribu kwa siku kadhaa kufikisha misaada katika taifa hilo bila ya mafanikio kutokana na vita vikali vya angani, majini na nchi kavu.

Marekani na Iran zajibizana

Marekani imeonya kuwa haitakaa na kuitizama Iran ikiwaunga mkono waasi wa Houthi huku kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khemenei akilaani kampeini ya kijeshi inayoongzwa na Saudi Arabia na kuitaja vitendo vya kihalifu na kutaka ikomeshwe mara moja.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/dpa/Karim Kadim

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito wa kurejea kwa mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kisiasa Yemen na kuonya mzozo huo huenda ukaaithiri kanda nzima.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 600, maelfu wamejeruhiwa na maelfu wengine wameachwa bila ya makaazi. Wakaazi wa Aden wamesema huduma za maji, umeme na ukusanyaji wa taka zimekatizwa mjini humo na hospitali zinashindwa kuhudumia idadi inayoongezeka ya waathiriwa wanaohitaji matibabu.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman