1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Othman Masoud ndiye makamu wa kwanza mpya wa rais Zanzibar

1 Machi 2021

Rais Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar amemteuwa aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa visiwa hivyo, Othman Masoud, kuchukua nafasi ya makamu wake wa kwanza kuchukuwa nafasi ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.

https://p.dw.com/p/3q3M2
Sansibar Othman Masoud Othman
Picha: DW/M. Khelef

Kulingana na taarifa kutoka Ikulu ya Zanzibar kuhusiana na uteuzi huo, baada ya Rais Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kushauriana na chama cha ACT Wazalendo, alimchagua Othman Masoud kuwa makamu mpya wa kwanza wa rais visiwani humo.

Sherehe ya kumuapisha rasmi itafanyika tarehe 2 Machi 2021 katika ukumbi wa Ikulu ya Zanzibar, ikiwa ni wiki mbili kamili tangu kufariki kwa Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alizitawala siasa za Zanzibar kwa takribani miaka 40.

Othman Masoud, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alikuwa ndiye mwendesha mashitaka mkuu wakati wa utawala wa Rais Amani Karume na kisha kuwa mwanasheria mkuu kwenye utawala wa Ali Mohamed Shein, lakini akafukuzwa kazi baadaye kutokana na msimamo wake uliopingana na wajumbe wa chama tawala cha Mapinduzi kwenye Bunge Maalum la Katiba mwala 2014. 

Mwandishi: Amina Abubakar