kuuawa Osama Bin Laden ndiyo suluhisho.
9 Desemba 2009Kamanda mkuu wa majeshi ya NATO nchini Afghanistan jenerali Stanley McChrystal amesema njia pekee ya kuwashinda magaidi wa Al-Qaeda ni kuuliwa au kukamatwa kwa Osama bin Laden.
Jenerali McChrystal amesema hayo leo mbele ya wabunge wa Marekani wakati akifafanua shabaha za uamuzi wa rais Obama wa kupeleka askari 30,000 zaidi nchini Afghanistan.
Jenerali McChrystal amesema ongezeko la askari litachangia katika kurudisha nyuma vuguvugu la Al-Qaeda hadi itakapofika wakati kama huu hapo mwakani na kuwatenga kabisa na wananchi wa Afghanistan.
Akifafanua mkakati mpya wa Marekani wa kuongeza majeshi nchini Afghanistan jenerali McChrystal alisema kwamba Osama bin Laden ndiyo mvuto wa Al-Qaeda kwa sasa,na kuendelea kwake kuishi kunawaimarisha Al-Qaeda hao na kuwawezesha kuwa na nguvu duniani.
Jenerali huyo amesema kuuawa au kukamatwa kwa Osama bin Laden hakutakuwa mwisho wa Al-Qaeda lakini ameeleza kwamba hafikiri iwapo itawezekana kuwashinda Al-Qaeda bila ya kuuawa au kukamatwa kwa Osama bin Laden.
Maafisa wa Marekani wanaamini kwamba Osama bin Laden anaesadikiwa kuwa alipanga mashambulio ya kigaidi ya terehe 11 mwezi septemba mwaka 2001nchini Marekani amejificha katika sehemu za milimani , kwenye mpaka baina ya Pakistan na Afghanistan.
Mshauri wa usalama wa taifa nchini Marekani James Jones alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba taarifa za upelelezi za hivi karibuni zinadokeza kuwa Osama bin Laden anaweza kuwa katika jimbo la Waziristan ya kaskazini- wakati mwingine katika upande wa Pakistan na wakati mwingine katika upande wa Afghanistan.
Hatahivyo waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates alisema katika mahojiano hivi karibuni kwamba Marekani haijui wapi Osama bin Laden anaweza kuwapo.
Jenerali Mchrystal amesema ana matumaini juu ya kuwashinda taliban nchini Afghanistan. Amesema hadi mwaka 2011 itakuwa wazi kwa watu wa Afghanistan kwamba taliban hawatashinda.
Mwandishi Mtullya Abdu/ AFPE
Mhariri/Abdul-Rahman