Osama Bin laden atoa vitisho dhidi ya Musharraf
21 Septemba 2007Mwito uliotolewa na Osama Bin Laden unahimiza vita vya jihad dhidi ya jenerali Pervez Musharraf wa Pakistan na serikali yake, jeshi lake pamoja na wale wote wanaoshirikiana nae.
Mwito huo umepuuzwa na utawala wa Pakistan, mshirika wa Marekani na serikali mjini Islamabad imesema kwamba haibabaiki na kitisho hicho licha ya kuwepo wasiwasi kuwa kundi la Al Qaeda limeanza tena kujikusanya karibu na maeneo ya mpaka wa Afghanistan.
Katika ukanda wa kunasa maneno uliotolewa jana na tawi la habari la mtandao wa kigaidi wa As- Sahab, imesadifu kwamba Bin Laden amewahimiza Wapakistani watimize vita vitakatifu dhidi ya rais Pervez Musharraf kwa ajili ya kushirikiana na Marekani katika vita dhidi ya wenye kuupigania Uislamu.
Ujumbe huo uliweza kuwafikia watu wengi hata ingawa haukupewa muda mrefu hewani na vyombo vya habari vya Pakistan.
Mara moja hali ilirejea katika ubishi kuhusu jenerali Musharraf na azma yake ya kugombea kwa mara nyingine tena wadhfa wake wa urais na pia hali ya ongezeko la bei za vyakula nchini Pakistan.
Swali linalo jitokeza hapa ni je, Pakistan inautoa muhanga hali tulivu ya usalama wake kwa kuchukua nafasi ya muda mrefu kama mshirika wa Marekani katika kampeni dhidi ya ugaidi.
Utawala nchini Pakistan umepuuza mwito huo wa Osama Bin Laden na kuhoji kwamba iwapo kweli Wapakistan wanamtii Bin Laden mbona hawakuitikia mwito wake na kutimiza alivyo taka.
Meja Jenerali Waheed Arshad msemaji wa jeshi la Pakistan amesema kuwa Osama Bin Laden hana wafuasi wengi nchini humo.
Nae msemaji wa rais Musharraf bwana Rashid Qureshi amefahamisha kwamba serikali itahakikisha kuwa Osama Bin Laden hapewi nafasi katika vyombo vya habari vya nchini humo na kwamba kujibu vitisho vya aina hiyo visivyokuwa na msingi ni sawa na kuvipa hadhi.
Marekani pia imesisitiza kuwa itaendelea kufanya kazi na mshirika wake Pakistan ili kuangamiza itikadi kali za kidini.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tom Casey amesema mjini Washington kuwa Bin Laden anaweza kundelea kutoa vitisho vyake kwa yeyote anaemtaka lakini Marekani itaendeleza juhudi zake pamoja na washirika wake wote bila hofu.
Pakistan inajitayarisha kufanya uchaguzi wa rais tarehe 6 mwezi ujao wa Oktoba.
Jenerali Pervez Musharraf hakabiliwi tu na vitisho kutoka kwenye kundi la Al Qaeda bali pia anakabiliwa na vizingiti vya kisheria dhidi ya azma yake ya kutaka kugombea tena kiti cha rais wa Pakistan.