Orban: Hungary ilikosea kushirikiana na utawala wa Kinazi
18 Julai 2017Ushirikiano wa Hungary na utawala wa Kinazi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia uliochangia kuangamizwa kwa Wayahudi, ulikuwa makosa na dhambi, kwani ilikosa kuwanusuru Wayahudi. Maneno hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban alipompokea Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyeko Hungary kwa ziara rasmi.
Victor Orban, amesema amemwambia Benjamin Netanyahu kuwa anafahamu historia ngumu waliyopitia, ambapo takriban Wayahudi laki tano na hamsini elfu wa Hungary waliuawa katika mauaji ya Holocaust.
Orban ameongeza kuwa awali, serikali ya Hungary ilifanya kosa na zaidi ilitenda dhambi iliposhindwa kuwalinda raia wa asili ya Kiyahudi, badala yake ilishirikiana na Wanazi, na kuwa hayo hayatarudiwa tena siku za baadaye.
Orban ameendelea kueleza kuwa: "Kuhusu ushirikiano, tumekubaliana sote kuwa ushirikiano wa Israel na Hungary ulenge mustakabali. Tumekubaliana kuwa usalama utakuwa muhimu zaidi. Nimempongeza Waziri Mkuu kutokana na juhudi zake na za Israel kwa usalama wa Ulaya."
Orban alisema hayo alipohutubia wanahabari baada ya mkutano wake na Netanyahu bungeni huku akisisitiza kuwa kila serikali inayo wajibu wa kuwalinda raia wake bila kujali asili yao.
Wakati wa uongozi wa Miklos Horthy ambaye alikuwa mshirika wa Adolf Hitler, Wayahudi nusu milioni kutoka Hungary walisafirishwa hadi kambi ya mauaji iliyosimamiwa na utawala wa Kinazi, na kuuawa.
Hungary, mtetezi wa Israel
Netanyahu ambaye ndiye Waziri Mkuu wa kwanza wa Israel kuitembelea Hungary tangu mwaka 1989 wakati Hungary ilipokuwa chini ya utawala wa kikomunisti, amesifia Hungary kwa kuiunga mkono Israel mara kwa mara na kuitetea dhidi ya kauli kinzani kutoka kwa wanaoikosoa sera za nchi hiyo ya Kiyahudi.
Netanyahu amesema ushirikiano wa nchi hizo mbili zitaendelea kwa manufaa ya siku za usoni. "Mustakabali ni kwa nchi ambazo zinavumbua. Israel ni taifa la uvumbuzi, Hungary ni nchi yenye vipaji tele na tunaamini ushirikiano huu kuendana na yale Waziri Mkuu ametaja, ninafikiri hii ndiyo mielekeo ya kusonga mbele."
Netanyahu na washirika zaidi kukutana
Hapo kesho, Netanyahu na Orban watakutana na viongozi wa Poland Jamhuri ya kidemokrasia ya Czech na Slovakia. Nchi hizo ni washirika wa Hungary katika kundi liitwalo Visegrad kando na kuwa ni nchi zinazowakilisha Wayahudi wa Hungary
Kampeni ya hivi karibuni ya serikali ya Hungary dhidi ya bwenyenye wa Marekani George Soros, ilizua ghadhabu za kimataifa, huku wakosoaji wakisema ilikuwa na matamshi ya chuki. Soros mwenye asili ya Hungary na kiyahudi ameyafadhili makundi mbalimbali yanayoikosoa mfumo wa utawala wa Orban, na pia dhidi ya sera za Netanyahu za Israel kukalia meneo ya Wapalestina.
Mwandishi: John Juma/DPAE/APE
Mhariri: Mohammed Khelef