1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Orban ashinda uchaguzi wa Hungary

9 Aprili 2018

Waziri Mkuu wa Hungary anayepinga sera za uhamiaji Viktor Orban ataongoza kwa muhula wa tatu mfululizo baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi. Uchaguzi huo ulifuatiliwa kwa karibu na mataifa ya Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/2vhT3
Ungarn Wahlen Viktor Orban Wahlsieg Jubel
Picha: Reuters/L. Foeger

Ushindi huo umewafurahisha viongozi wengine wa siasa kali za kizalendo lakini huenda ukasababisha tumbo joto katika baadhi ya nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya: Akiwahutubia wafuasi wake mjini Budapest jana usiku, Orban aliyaita matokeo hayo kuwa ni ''ushindi wa kuamua hatima'' ambao utawapa Wahungary ''fursa ya kujilinda wenyewe na kuilinda Hungary''.

''Ningependa kuwaambieni kuwa mapambano makubwa yamekwisha. Tumepata ushindi mkubwa. Tumeweka fursa ya kuilinda Hungary. Nchi yetu ya Hungary, haiko mahali ambapo tungependa kuiona, lakini sasa imeelekea kwenye barabara ambayo imejichagulia yenyewe. Tutaifuata barabara hii pamoja. Ahsanteni kwa kila kitu''.

Ungarn Parlamentswahl 2018 | Auszählung der Stimmen
Matokeo kamili ya kura yatatolewa baada ya siku kadhaaPicha: Reuters/L. Foeger

Chama cha Orban cha Fidesz kilishinda karibu asilimia 49 ya kura, ikiwa ni matokeo yaliyoboreshwa kwa kulinganishwa na ya miaka minne iliyopita na ambayo huenda yakakipa wingi wa theluthi mbili ya viti bungeni, jambo ambalo linaweza kukisaidia kuirekebisha katiba.

Baadhi ya wanachama wa Umoja wa Ulaya huenda wakauangalia kwa hofu umaarufu wa Orban ndani ya nchi yake, ukizingatia mkwaruzano wake wa kila mara na taasisi za umoja huo kuhusu sera zake kali za kupinga uhamiaji na kuukataa mpango wa Umoja wa Ulaya wa kugawana wakimbizi, pamoja na hatua zake kuyakandamiza makundi ya kiraia.

Hata hivyo, viongozi wa siasa kali za kizalendo na wale wa siasa kali za mrengo wa kulia ambao wanavutiwa na aina ya siasa za utambulisho za Orban na madai ya kuwa mlinzi wa kile anachokiita kuwa ni ''Ulaya ya Kikristo'' watapata amani na matokeo hayo.

Katika hotuba yake jana usiku, Orban mwenyewe alimshukuru Jaroslaw Kacynski, kiongozi wa chama tawala nchini Poland cha PiS, kwa msaada wake.

Ungarn | Anti-Soros Plakate
Bango la kumpinga Soros nchini HungaryPicha: AFP/Getty Images

Poland na Hungary wanajiona kuwa washirika wakuu katika mapambano yao dhidi ya taasisi za Umoja wa Ulaya. Kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Ufaransa Marine Le Pen na mwenzake wa Uholanzi Geert Wilders walikuwa wa kwanza kutuma ujumbe wa pongezi baada ya matokeo hayo kuwa wazi.

Uchaguzi huo umethibitisha nguvu za Orban ndani ya nchi na kudhihirisha wazi udhaifu na mparaganyiko unaoendelea kuukumba upinzani. Chama kilichotoa ushindani mkubwa kwa Fidesz, cha Jobbik, ambacho ni cha siasa kali za mrengo wa kulia kilipata asilimia 20 ya kura.

Serikali ya Orban tayari imesababisha utata kwa kile wakosoaji wanasema kuwa ni kukandamiza uhuru wa habari na mahakama, pamoja na msako wake dhidi ya mashirika ya kiraia, na hasa wale wenye mahusiano na bilionea wa Marekani mzaliwa wa Hungary, mliberali George Soros.

Serikali imetuhumiwa kwa kuendesha kampeni isiyo na kikomo dhidi ya Soros, ambaye ni Myahudi. Orban anamtuhumu Soros na mashirika anayoyafadhili kwa kuunga mkono mmiminiko wa wahamiaji wa Kiislamu na Kiafrika kuingia Ulaya ili kuhujumu utambulisho wake wa Ukristo.

Matokeo kamili ya uchaguzi huo wa jana yatatolewa baada ya siku kadhaa, wakati kura zote zilizotumwa na Wahungary wanaoishi ng'ambo na Wahangury wanaoishi katika nchi jirani zitakapohesabiwa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo