Bunge la Ulaya kuamua juu ya mienendo ya Hungary
12 Septemba 2018Kura hiyo itakayopigwa Jumatano katika Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, inafuatia ripoti ya mbunge Judith Sargentini kutoka Uholanzi, ambayo imeelezea kwa kina jinsi serikali ya Hungary inayoongozwa na chama cha mrengo mkali wa kulia cha Waziri Mkuu Viktor Orban inavyokiuka maadili muhimu ya Umoja wa Ulaya. Ripoti hiyo inaituhumu Hungary kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na wasomi, kuwafukua kazi majaji wanaofanya kazi kwa uhuru, kuzinyanyasa asasi za kiraia, na kuendeleza ubadhirifu.
Hatua dhidi ya nchi inayokwenda kinyume na maadili ya msingi wa Umoja wa Ulaya huchukuliwa kulingana na kifungu nambari 7 cha mkataba wa umoja huo, na hadi sasa imekwishaidhinishwa dhidi ya nchi moja tu, Poland ambayo kama Hungary inaongozwa na chama chenye sera kali za uzalendo.
Orban ayakunjua makucha yake Strasbourg
Hapo jana, Viktor Orban alifika katika bunge la Ulaya, ambapo alilishambulia bunge hilo akisema nchi yake inalengwa kwa sababu imepinga sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu wahamiaji.
''Kwa heshima zote lakini pia kwa uthabiti, napinga mpango wa wale wanaunga mkono wahamiaji ndani ya Umoja wa Ulaya, kuwatisha na kuwachafua wa-Hungary kwa misingi ya uongo. Kwa heshima, nawaaifu kuwa hatua zozote mtakazozichukua, Hungary haitatii vitisho vyenu, itailinda mipaka yake dhidi ya wahamiaji haramu, na italinda haki zake, ikibidi, dhidi yenu''. Alisema.
Hotuba yake kali ya dakika tano ilijibiwa na wabunge, wengi wakipinga hoja yake kwamba Hungary inaonewa kutokana na msimamo wake. Judith Sargentini aliyeongoza uchunguzi kuhusu nchi hiyo, alisema serikali ya Viktor Orban inasimamia mmomonyoko wa utawala wa sheria.
Wabunge wamshambulia, mmoja baada ya mwingine
Makamu wa kwanza wa rais wa Kamisheni ya Ulaya, Frans Timmermans aliishutumu serikali ya Hungary kuvitisha vyama vya kiraia, ambavyo alisema ndio msingi wa utawala wa kidemokrasia.
Kiongozi wa wabunge wa vyama vya kihafidhina katika bunge la Ulaya, mjerumani Manfred Weber, alimshauri Viktor Orban na serikali yake kuchagua kati ya Umoja wa Ulaya, na kujifungia katika siasa za utaifa.
Mkuu wa vyama vya kiliberali katika bunge hilo, Guy Verhofstadt wa Ubelgiji alimweleza wazi Orban kwamba sera zake hazifai ndani ya Umoja wa Ulaya.
''Hebu tuambiane ukweli, ukweli mchungu ni huu: Hungary ingeongozwa na sera zako wakati ikiomba kuingia katika Umoja wa Ulaya, isingekaribishwa. Huo ndio ukweli.'' Alisema Verhofstadt.
Lakini si wote waliompinga waziri mkuu huyo wa Hungary. Vyama vya mirengo mikali ya kulia, kikiwemo cha Mbadala kwa Ujerumani AfD, na mwanasiasa aliyeongoza mchakato wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya Nigel Frage, walikuwa maswaiba wake.
Muungano wa vyama vya sera za wastani za mrengo wa kulia, ambao chama cha Orban ni mwanachama wake, ndio utaamua ikiwa kura dhidi ya Hungary itapita au la. Muungano huo, EPP, umegawanyika katika mitazamo yake kuhusu shutuma dhidi ya nchi hiyo.
Mwandishi: Bernd Riegert/Daniel Gakuba/dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga