1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Opereshini za kijeshi za Ufaransa

15 Januari 2013

Operesheni za kijeshi za Ufaransa nchini Mali na kishindo cha kucheleweshwa ufunguzi wa kiwanja cha ndege cha Berlin ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini .

https://p.dw.com/p/17KAu
Ndege ya kivita ya Ufaransa chapa RafalePicha: Reuters

Tuanzie lakini Mali. Wahariri wanakubaliana mshikamano ni muhimu ili kuzuwia kitisho cha kusonga mbele wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislamu,lakini hatima ya opereshini hizo je ikoje? Gazeti la "Schweriner Volkszeitung" linaandika:

Operesheni za umwagaji damu za kijeshi na uchokozi unaotisha wa waasi kuonyesha picha za wanajeshi waliouliwa wa kifaransa, unabainisha wazi kabisa kwamba hatima na matokeo ya opereshini hizo hakuna ayajuaye. Serikali kuu ya Ujerumani inapoahidi kumsaidia jirani na mshirika wake wa dhati ikiondowa wakati huo huo lakini uwezekano wa kuchangia kijeshi, hali hiyo inamfanya mtu aingiwe na hofu na kujiuliza kama opereshini hizo kweli zitafanikiwa. Pengine kwa kipindi cha muda mfupi ujao, opereshini za kijeshi za Ufaransa zitawazuwia wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislamu na al Qaida wasiiteke Mali, lakini kwa mtazamo wa muda mrefu, opereshini hizo za kijeshi sio ufumbuzi. Pale tu ambapo Umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya watakapoamua haraka na kuwajibika ndipo pengine litakapoepukwa balaa kwa Ufaransa na washirika wake kuiona Mali ikigeuka Afghanistan ya pili.

Chanzo halisi cha mzozo kifumbuliwe

Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linaandika:"Rais Francois Hollande wa Ufaransa anajijenga kama kiongozi jasiri wa kijeshi anayetetea masilahi ya Ufaransa ulimwenguni. Hata hivyo uungaji mkono wa operesheni hizo za kijeshi nchini Mali usituhadae. Hollande anapambana na dalili tu na sio vyanzo. Wadadisi wote wanakubaliana kuna uwiano kati ya shida za kiuchumi na udhaifu wa watu kushawishika na matamshi ya itikadi kali. Mwenye kufanya kazi na kuwa na matumaini, matamshi kama hayo hayamshughulishi. Matokeo ya opereshini ya kijeshi hakuna ajuaye. Kinachojulikana kwa uhakika ni kwamba ufumbuzi, kama utapatikana, basi utakuwa wa muda tu."

Platzeck ayatia rehani maisha yake ya kisiasa

Ministerpräsident Matthias Platzeck Vertrauensfrage im Landtag Brandenburg
Waziri mkuu Matthias Platzeck akikabiliana na kura ya kutokuwa na imani nae katika bunge la BrandenburgPicha: dapd

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Berlin ambako kasheshe ya kukawilishwa ufunguzi wa uwanja wa ndege wa "Berlin-Brandenburg" imepelekea meya wa jiji la Berlin, Klaus Wowereit, kuacha wadhifa wake kama mwenyekiti wa baraza la usimamizi la ujenzi wa uwanja huo wa ndege na jana waziri mkuu, Matthias Platzeck, kusalimika na kura ya kutokuwa na imani naye bungeni. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung "linaandika:Ni hatari pale Platzeck anapofungamanisha hatima yake ya kisiasa na kufanikiwa mradi wa ujenzi wa uwanja huo wa ndege. Kwa sababu kasheshe hiyo ni kubwa kwa namna ambayo hakuna anayeweza kuashiria lini uwanja huo wa ndege utaanza shughuli zake. Huenda pengine uchaguzi wa jimbo utakapoitishwa mwakani huko Brandenburg, Platzeck akaondolewa patupu. Sababu hazikosekani ikikumbukwa kwamba tangu zamani amekuwa mwanachama wa baraza la usimamizi na kwa hivyo anabeba jukumu la kasheshe hiyo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo