Polisi wakabiliana na wahamiaji mjini Casablanca
18 Januari 2023Imetokea purukushani baina ya polisi na wahamiaji katika mji wa Casablanca nchini Moroko, wakati polisi walipotaka kuwaondoa wahamiaji hao katika kambi isiyokubaliwa kisheria.
Duru za vyombo vya habari katika eneo hilo zimeeleza kuwa wahamiaji hao ambao wanatoka kusini mwa jangwa la Sahara waliwarushia mawe polisi na kuyachoma moto magari kupinga operesheni ya kuwafurusha.
Moroko ni njia inayopendelewa na wahamiaji wanaokimbia umasikini na vurugu katika mataifa yao wakiazimia kuhamia Ulaya kupitia bahari ya Mediterania au pwani ya nchi hiyo kwenye bahari ya Atlantiki. Kwa mujibu wa tovuti ya shirika la habari la umma la SNRT, afisa mmoja wa polisi amejeruhiwa, na magari matano yaliteketezwa kwa moto katika vurugu hizo.
Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Moroko la AMDH limelaani ukandamizaji wa polisi katika operesheni yake kwenye kambi hiyo ya wahamiaji.