Operesheni ya kuwasaka wanamgambo yaendelea Mali
14 Februari 2013Hii inakuja siku moja tu baada ya Urusi kufichua kuwa inaipa serikali ya Mali silaha, wakati wanajeshi wa Ufaransa wakitegua bomu kubwa kaskazini mwa nchi hiyo. Mkuu wa shirika la Urusi la kuuza silaha katika nchi za kigeni amesema amekabidhi silaha ndogondogo kwa serikali hiyo ya Afrika Magharibi ambayo haina silaha za kutosha na yenye jeshi lililogawanyika. Katikati ya mji wa kaskazini wa Gao, eneo ambalo kulitokea miripuko miwili ya bomu na makabiliano makali ya ardhini katika siku chache zilizopita, wanajeshi wa Ufaransa jana wamelitegua bomu la kujitengenezea ambalo wamesema lilikuwa na uzani wa kilo 600.
Bomu hilo lilipatikana katika jumba moja lisilokaliwa na watu na inaaminika lilikuwa hapo tangu Jumatatu wiki hii. Umoja wa Mataifa umesema unatengeneza mkakati wa kikanda katika eneo la Sahel. Wachambuzi wanasema mchanganyiko hatari wa uasi wa kiislamu wenye itikadi kali, utekaji nyara, ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu wa kupangwa unachangia katika machafuko yanayoshuhudiwa katika eneo hilo.
Jeshi la Mali linapambana kureesha usalama baada ya jeshi linaloongozwa na Ufaransa kusaidia kuwatimua waasi walio na mafungamano na mtandao wa al-Qaeda ambao walikuwa wameudhibiti upande wa kaskazini ya nchi hiyo. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Sahel Romano Prodi, na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Afrika Magharibi Said Djinnit wanafanya ziara ya siku tatu katika eneo hilo ili kujadili hali nchini Mali na marais wan chi jirani za Senegal, Mauritania, Burkina Faso na Niger. Mkuu wa Haki za binadaamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay ameonya kuwa Mali inakabiliwa na kitisho na kutumbukia katika wimbi la machafuko.
Anasema tatizo siyo tu makundi ya waasi lakini pia jeshi, na weusi walio wengi ambao wamefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya WaTuareg walio weupe na Waarabu wanaoshutumiwa kwa kuunga mkono uasi. Makundi ya haki za binadamu yanalishutumu jeshi la Mali kwa kuwauwa washukiwa wa uasi na kuitupa miili yao kwenye visima. Watuareg na Waarabu pia wanashambuliwa na jirani zao weusi katika miji ya kaskazini kama vile Timbuktu.
Mgogoro wa Mali umewalazimu takribani watu 337,000 kutoroka makwao ikiwa ni pamoja na watu 150,000 ambao wametafita hifadhi nje ya mipaka ya Mali kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Ufaransa ilizindua operesheni yake ya kijeshi mnamo Januari 11 baada ya serikali ya mpito ya Mali kuomba usaidizi baada ya kuanza kuzidiwa nguvu na wanamgambo. Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa mwezi Machi Kapteni Amadou Sanogo, ameapishwa jana mjini Bamako kama mkuu wa kamati ya mageuzi ya kijeshi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo