1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yatangaza operesheni dhidi ya IS Anbar

26 Mei 2015

Iraq imetangaza kuzinduliwa kwa operesheni ya kuukomboa mkoa wa Anbar ambako wapiganaji wa Dola ya Kiislamu IS waliteka mji mkuu mwezi huu, katika pigo kubwa kwa juhudi za Marekani kulitokomeza kundi hilo la Kisunni.

https://p.dw.com/p/1FWOV
Irak Ramadi Angriff
Picha: picture-alliance/dpa/A. Al-Shemaree

Kundi la Dola ya Kiislamu limeripotiwa kupeleka wapiganaji zaidi katika mji wa Ramadi, kujiandaa na mapambano hayo, huku Marekani ikihangaika kuihakikishia ushirikiano serikali mjini Baghad, baada ya afisa wa Marekani kuvikosoa vikali vikosi vya Iraq.

Waasi wa Dola ya Kiislamu au Daesh kama wanavyojulikana kwa Kiarabu walijiimarisha mjini Ramadi siku ya Jumatatu, kwa kupeleka wapiganaji zaidi kujiandaa na vita dhidi ya majeshi ya usalama na makundi ya wanamgambo yanayosonga mbele kuelekea mji mkuu huo wa jimbo la Anbar, uliopo umbali wa kilomita 110 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Vikosi vya Iraq vimerejesha baadhi ya maeneo mashariki mwa Ramadi tangu kuanzisha mashambulizi siku ya Jumamosi, wiki moja baada ya kufurushwa na IS, na jana Jumatatu vilichukuwa eneo la vijiji kusini mwa mji huo.

Mpiganaji wa Kishia akiwa tayari kwa mapambano dhidi ya IS mkoani Anbar.
Mpiganaji wa Kishia akiwa tayari kwa mapambano dhidi ya IS mkoani Anbar.Picha: Getty Images/J. Moore

Operesheni kuhusisha makundi mbalimbali

Kamanda wa operesheni za Mto Euphrates Meja Jenerali Qais Al Muhammadawi, amesema mashambulizi ya kuikomboa Ramadi yatahusisha jeshi la Iraq, wanamgambo wa Kishia na wapiganaji wa Kisunni. "Ni eneo muhimu sana. Tuna idadi nzuri tu ya watu wanaolifahamu, marafiki wanalijua, makabila, jeshi, polisi, PMF, wote na sisi wote kundi hili linalopambana dhidi ya adui Deash," alisema Muhammadawi.

Wakaazi wa Ramadi waliripoti kuwa magari yaliyobeba wapiganaji wa Dola ya Kiilsamu yaliwasili mjini humo siku ya Jumapil, na kuanza kuwatawanya kwenye maeneo mbalimbali. Abu Saed alisema aliwaona wapiganaji wa IS wakishuka kwenye magari mawili na kukimbilia kwenye majengo na kujificha. Mkaazi mwingine alisema aliona wapiganaji wasiopungua 40 wakiruka kwenye magari yaliyowasili katika wilaya ya kusini ya al-Tamim Jumapili jioni.

Katika matamshi aliyoyatoa kwa televisheni ya CNN siku ya Jumapili, waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter, alivikosoa vikosi vya Iraq kwa kushindwa kuidhibiti Ramadi, licha ya kuwa na idadi kubwa kuliko wapiganaji wa IS. Matamshi hayo yalijibiwa kwa hasira na waziri mkuu wa Iraq, Heider Al.Abadi, ambaye aliliambia shIrika la utangazaji la Uingereza BBC, kuwa waziri huyo wa ulinzi wa Marekani alipewa taarifa zisizo sahihi. Abadi alitabiri kuwa Ramadi itarejeshwa mikononi mwa serikali katika "muda wa siku tu."

Vikosi vya usalama vya Iraq vilipoondoka mjini Ramadi, kukimbia moto wa IS.
Vikosi vya usalama vya Iraq vilipoondoka mjini Ramadi, kukimbia moto wa IS.Picha: picture alliance/AP Photo

Marekani yahaha kurekebisha hali

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden alizungumza na Abadi jana, na taarifa ya ikulu ya White House ilisema Biden alitambua kujitolea kwa kiwango kikubwa na ushujaa wa vikosi vya Iraq katika kipindi cha miezi kumi na nane iliyopita mjini Ramadi na kwingineko, na kuongeza kuwa Marekani itafanya kila iwezelo kuvisaidia vikosi vya Iraq, yakiwemo makabila ya mkoa wa Anbar, ili kuwaondoa magaidi wa IS mkoani humo.

Kutekwa kwa mji wa Ramadi na mji wa kale ya Palmyra nchini Syria, ndiyo mafanikio makubwa zaidi ya IS tangu muungano unaoongozwa na Marekani ulipoanzisha mashambulizi ya angani dhidi yao mwaka uliopita. Ushindi wa karibu wakati mmoja dhidi ya majeshi ya Iraq na Syria umeilaazimu Marekani kutafakari upya mkakati wake wa mashambulizi ya angani, huku ikiacha mapigano ya ardhini kwa vikosi vya Iraq.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,aptn

Mhariri: Daniel Gakuba