1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OPCW yaunga mkono uchunguzi wa Uingereza

12 Aprili 2018

Shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za sumu, OPCW limethibitisha matokeo ya uchunguzi yaliyotolewa na Uingereza kuhusu aina ya sumu ya kuua neva iliyotumika katika shambulizi dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi.

https://p.dw.com/p/2vwsB
OPCW Logo der Organisation für das Verbot von Chemiewaffen
Picha: picture-alliance/ANP/dpa/E. Daniels

Shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za sumu, OPCW hii leo limethibitisha matokeo ya uchunguzi yaliyotolewa na Uingereza kuhusu aina ya sumu ya kuua neva iliyotumika katika shambulizi dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi, ambayo Uingereza ilisema ilitokea Urusi. 

Shirika hilo la kimataifa la kudhibiti silaha za sumu la OPCW limesema sampuli zilizopimwa zimethibitisha matokeo ya uchunguzi yaliyotolewa na Uingereza kuhusiana na aina ya sumu iliyotumika dhidi ya jasusi huyo.

Hata hivyo, OPCW haikueleza kuhusu nani anayetakiwa kulaumiwa kwa shambulizi la Machi 4, ambalo pia lilimuathiri binti ya jasusi huyo Yulia Skripal na polisi wa eneo lilipotokea shambulizi hilo. 

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson amesema Uingereza itahitaji majibu kutoka Urusi baada ya ripoti ya OPCW ambayo kimsingi inaunga mkono tuhuma kwamba ilihusika na shambulizi hilo la sumu ya kuua mishipa ya neva dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi, Sergei Skripal nchini Uingereza. Ripoti hii ni kulingana na uthibitisho wa sampuli zilizopimwa kwenye maabara nne huru na zinazoheshimika zaidi duniani. 

Johnson amesema ripoti hiyo inathibitisha kwamba sumu hiyo ya Novichok iliyotengenezwa Urusi, ndio iliyotumika kwenye shambulizi la mwezi uliopita, na kwamba hakuna mashaka yoyote kuhusu kile kilichotumiwa na hakuna haja ya maelezo zaidi kuhusu nani aliyehusika. 

Großbritannien Boris Johnson in London
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson amesema hakuna haja ya ushahidi mwingine kwamba Urusi ilifanya shambulizi hilo.Picha: Reuters/H. McKay

Urusi yasema haitazungumza chochote hadi itakaposoma ripoti ya OPCW.

Amesema watashirikiana bila kuchoka na washirika wao katika kuzuia matumizi ya silaha kama hizo, lakini pia tayari wameitisha kikao cha halmashauri kuu ya OPCW Jumatano ijayo ili kujadiliana hatua zitakazofuata, huku taarifa nyingine zikisema Uingereza pia imeomba kikao na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa cha kuijadili ripoti hiyo, na kulingana na ujumbe wa Uingereza kwenye Umoja huo, kikao hicho kinatarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Kwenye mkutano kuhusu masuala ya uhalifu wa kimtandao mjini Manchester, mkuu wa shirika la kijasusi la Uingereza, GCHQ Jeremy Fleming akizungumza kwa mara ya kwanza mbele ya hadhara tangu aliposhika wadhifa huo mwaka jana amesema shambulizi hilo lililofanywa na Urusi lilikuwa ni baya na la kushtusha. 

Shirika la habari la serikali la Urusi, TASS limeripoti kwamba naibu waziri wa wizara ya mambo ya nje Sergei Ryabakov amesema Urusi itahitaji kuisoma kwanza ripoti hiyo ya OPCW, kabla haijatoa maoni yake. Aidha msemaji wa wizara hiyo Maria Zakharova amesema Uingereza inatakiwa kuthibitisha kama haiwashikilii mateka Skripal na binti yake Yulia, kwa madai kuwa wametengwa na serikali ya Uingereza na hakuna aliyewaona kwa zaidi ya mwezi mmoja.  

Nchini Ujerumani, wizara ya mambo ya kigeni kupitia msemaji wake imeitaka Urusi kutoa majibu ya maswali ya wazi kuhusu shambulizi hilo la sumu baada ya ripoti hiyo ya OPCW, huku ikiikaribisha hatua ya Uingereza ya kukihusisha chombo hicho cha kimataifa kuanzia mwanzo, pamoja na mwito wa kikao maalumu na shirika hilo.  

Urusi tangu awali ilikana kufanya shambulizi hilo, hatua iliyoibua mzozo wa kidiplomasia kwa kuwafukuza wanadiplomasia kutoka pande zote.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/DPAE/AFPE/RTRE.
Mhariri: Iddi Ssessanga