1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMarekani

Onyo la baridi kali latolewa kwa watu milioni 200 Marekani

24 Desemba 2022

Zaidi ya watu milioni 200 nchini Marekani wametahadharishwa kufuatia baridi kali. Hayo yamesemwa na shirika la taifa hilo la utabiri wa hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/4LOFC
Wetter in den USA
Picha: Travis Heying/The Wichita Eagle via AP/picture alliance

Mamilioni ya Wamarekani wanakabiliwa na baridi kali huku viwango vya joto vikirekodiwa hadi 56 chini ya sifuri katika vipimo vya Celcius.

Watu wengi wamelazimika kuahirisha safari na mipango yao ya sherehe za Krismasi mnamo wakati asilimia 60 wa wakaazi nchini humo wakionywa kusalia majumbani.

Marekani yakumbwa na dhoruba kali zaidi ya baridi baada ya kipindi cha miaka 30

Kulingana na tovuti ya PowerOutage inayofuatilia huduma za umeme nchini humo, dhoruba hiyo ya baridi kali imesababisha umeme kukatika katika baadhi ya maeneo na kuwaacha zaidi ya watu milioni moja gizani, hususan kutoka kusini na mashariki mwa nchi hiyo.

Karibu ndege 5,000 za ndani nchini Marekani zimelazimika kufuta safari zao, hali ambayo imevuruga mipango ya wengi waliotaka kusafiri msimu huu wa Sikukuu.

Wataalam wa utabiri wa hali ya hewa wamesema kuna baridi kali sana hivi kwamba katika maeneo mengine kutoka nje kunaweza kusababisha joto kushuka kupita kiasi mwilini au hata vifo.

Zaidi ya safari 5,000 za ndege Marekani zimefutwa kwa sababu ya hali mbaya ya hewa
Zaidi ya safari 5,000 za ndege Marekani zimefutwa kwa sababu ya hali mbaya ya hewaPicha: Nam Y. Huh/AP Photo/picture alliance

"Ikiwa kuna baridi shadidi kiasi hiki, mtu huweza kujipata taabani,” Rich Maliawco ambaye ni mtabiri wa hali ya hewa ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.

Hali ya hatari kwenye barabara inazidi kuenea wakati ambapo Wwamarekani zaidi ya milioni 100 walikuwa wanatarajiwa kwenda kwenye shughuli zao za kila siku. Theluji nzito imeanguka na kufunika barabara na kufanya baadhi yazo kutopitika kabisa.

Mnamo Alhamisi watu wawili waliripotiwa kufariki kufuatia ajali ya barabarani katika jimbo la Oklahoma na kule Kansas watu watatu pia walifariki kwenye ajali ya barabarani.

Waziri wa Uchukuzi Pete Buttiegieg alionya kwamba safari za Krismasi zinaathiriwa zaidi na dhoruba hiyo.

Gavana wa New York ameungana na magavana wa majimbo mengine kutangaza hali ya dharura na ametahadharisha juu ya hatari ya kutokea maafa.

Taarifa iliyotolewa imetahadharisha juu ya uwezekano mkubwa wa kutokea mafuriko mgando wa barafu miongoni mwa athari nyinginezo.

Chanzo: APE,AFPE